- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
ASKOFU MAGONZA: KUNAWATU WAMEVAMIA MAKANISA WAKIJIFANYA KUTETEA WANYONGE
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amewaonya vikali wanasiasa wanaotumia mwamvuli wa kutetea wanyonge kwa lengo la kujinufaisha kisiasa, kiuchumi na kiitikadi.
Katika mahubiri aliyoyatoa jana kwenye ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Lukajambe wilayani Karagwe mkoani Kagera, Dk Bagonza pia alionya watu wanaoshabikia vitendo vya umwagaji wa damu.
“Niweke angalizo. Unyonge wetu, maradhi yetu, umaskini wetu si mtaji wa wasaka tonge. Bwana Yesu hakunufaika na mateso yale, tulionufaika ni sisi,” alisema Dk Bagonza.
“Kwa hiyo wanaojitoa kutetea wanyonge wawe makini kutoutumia unyonge wetu kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kiitikadi na hata kiimani.”
Alisema kuna watu wamevamia hata kwenye ibada wakijifanya kutetea wanyonge kumbe siyo kweli.
“Unakuta mtu anakazana kutetea wanyonge, lakini ukimwangalia kwa makini, ana lake. Ni kama anataka tuendelee kuwa wanyonge ili apate kazi. Bwana Yesu alichukia unyonge wetu, bila hivyo asingekwenda msalabani,” alisisitiza.
“Wapatikane watu watakaokubali kuteseka kupinga unyonge huu, watukanwe waitwe majina mabaya, waandikwe magazetini na mitandaoni, watishiwe maisha yao, wazushiwe maisha yao, lakini wajue kuwa Mungu hawezi kuwaacha kwa sababu hakumwacha mwana wake pale msalabani.”
Akizungumzia umwagaji wa damu, Dk Bagonza alisema huwa haimwagiki bure, bali huleta ukombozi au huangamiza.
Alisema, “tuwe macho, kwa sababu kutukuza, kushabikia, kukalia kimya umwagaji wa damu isiyo na hatia kuna madhara makubwa.”
“Isipofanya hivyo inaangamiza. Waweza usiangamie wewe unayeshabikia, waweza usiangamie uliyekaa kimya, wakaja kuangamia uzao wako au Taifa lako na hawa hawakuwa na hatia kwa sababu hawakuwepo wakati wewe unakumbatia umwagaji damu.”
Akizungumzia upendo kwa ajili ya wengine, aliwataka waumini na Watanzania kujitolea kwa wengine, huku pia akitoa mifano ya Tanzania kujitolea kwa ajili ya uhuru wa nchi nyingine.
“Kujitoa na kujitolea ni mambo yanayoanza kupotea kwenye kanisa na kwenye Taifa letu, tujitoe nafsi yetu kwa ajili ya kanisa na Taifa letu.
“Nakumbuka nikiwa shule ya msingi katikati ya miaka ya 1970 tuliambiwa tujitolee damu halafu inapelekwa Msumbiji, chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni pale tulipotangaza kuwa uhuru wetu hauna maana kama bado nchi za wenzetu hazijawa huru.”
Alisema katika kuonyesha upendo, Tanzania iliguswa na mateso waliyopata wananchi wa Uganda kutokana na utawala wa kidikteta.
“Sisi wa Mkoa wa Kagera tunakumbuka jinsi Taifa letu lilivyotumia gharama kubwa likaingia vitani kupinga udikteta katika nchi jirani. Ulihusu nini ule udikteta? Sisi hatukuwa na udikteta tulikuwa tunaishi vizuri. Lakini tuliona uhuru wetu hauko sahihi ikiwa kuna jirani yetu anateseka,” alisema.
Dk Bagonza aliyesoma maandiko ya Biblia katika Kitabu cha Mathayo 27:27-31, 39-41 alisema lengo la Yesu kuteswa msalabani lilikuwa ni upendo wa Mungu kwa wanadamu.
“Sisi Wakristo tunaamini tendo hili linasimama katika misingi miwili. kwanza ni upendo; Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee awe sadaka kwa ajili yetu. Hata kama Yesu hakupenda, bali alikubali kwa unyenyekevu mkuu. Siyo misumari tu iliyomzuia Yesu msalabani bali ni upendo.”