- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
AFYA: IFAHAMU TEZI DUME NA TIBA YAKE
Kansa ya tezi dume ni aina ya kansa ambayo huwapata wanaume tu. Kansa hii hutokea katika tezi maalumu zilizopo kwa mwanaume ziitwazo Tezi za kibofu. tezi hizi hupatikana katika mfumo wa uzalishaji wa mwanaume.
Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume wa umri mbalimbali duniani hasa wenye miaka kuanzia 50.
Aidha ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wa umri miaka 70 na kuendelea. Hata hivyo, ni nadra sana kwa saratani hii kuwapata wanaume chini ya miaka 40.
Nani yupo katika hatari ya kupata saratani ya tezi dume?
Watu walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na:
- Wanaume wenye asili ya Afrika (weusi) ikilinganishwa na wazungu
- Wanaume kuanzia miaka 60 na kuendelea
- Wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zake (kaka au mdogo wa kiume) au baba amewahi kuugua ugonjwa huu.
- Wanaume wanaokunywa pombe kupindukia
- Wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza rangi au wanaofanya kazi ya kupaka rangi
- Wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali
- Wanaofanya kazi katika viwanda vya utengenezaji matairi
- Wachimbaji wa madini hususani aina ya cadmium
- Walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama
Pamoja na kwamba, tatizo la kukua na kuongezeka kwa tezi dume yaani BPH hutokea kwa wanaume wengi, hali hiyo haiongezi uwezekano/hatari ya kupata saratani ya tezi dume.
Dalili za saratani ya tezi dume ni zipi?
Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani sana na zile za kuvimba kwa tezi dume (BPH). Dalili hizo ni pamoja na
- Kupata shida unapoanza kukojoa
- Kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa
- Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu
- Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku
- Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote
- Kutoa mkojo uliochanganyika na damu
- Kutoa shahawa zilizochanganyika na damu
Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu za jirani ya mwili, mgonjwa anaweza kuwa na
- Maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni
- Uume kushindwa kusimama (uhanithi)
- Aidha, mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu n.k
Vipimo gani vitathibitisha kuwa nina saratani ya tezi dume?
Utambuzi wa saratani ya tezi dume hujumuisha kufahamu historia ya mgonjwa pamoja na familia yake, kufahamu dalili alizo nazo mgonjwa pamoja na kufanya vipimo kadhaa. Vipimo vinavyoweza kufanywa ni pamoja na
- Digital rectal exam: Daktari ataingiza kidole cha shahada katika puru (rectum) ili kuhisi tezi dume kupitia ukuta wa puru. Aidha atahisi pia sehemu zote zinazozunguka tezi dume kutambua iwapo tezi ni ngumu au kama ina uvimbe wowote.
- Kipimo cha damu kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume. Uzalishaji wake huongezeka wakati wa BPH, tezi dume inapopata uambukizi (prostitis) , na saratani ya tezi dume.
DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au BPH. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa.
- Prostate biopsy: Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua kipande cha nyama (tishu) kutoka tezi dume kwa ajili ya uchunguzi maabara.
Kipimo kingine huitwa transrectal ultrasound ambacho husaidia kuonesha ukubwa na sura ya tezi dume lilivyo.
Ili kutambua kama saratani imesambaa sehemu nyingine za mwili vipimo vya CT scan, MRI pamoja na PET navyo vyaweza kufanyika pia.
Saratani ya tezi dume inatibika?
Ndiyo! Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika.
Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi, wakati kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri kumfuatilia mgonjwa kwa ukaribu bila kumfanyia upasuaji au bila kumpatia tiba ya mionzi.
Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu (hormonal therapy), au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).
Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa walio katika hatua za awali za ugonjwa (stage I na stage II) ingawa pia hufanywa kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu yaani stage III na stage IV. Upasuaji unaofanywa ni ule wa kuondoa tezi dume pamoja na baadhi ya tishu zinazozunguka tezi hiyo.
Tiba ya Mionzi
Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi kuua seli zenye saratani. Tiba ya mionzi hutumika kutibu saratani ya tezi dume ambayo haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili. Aidha inaweza pia kutumika kuua masalia ya tishu zenye saratani mara baada ya kufanyika kwa upasuaji.
Kwa wagonjwa walio katika hatua ya mwisho ya saratani yaani wale ambao saratani tayari imeshasambaa mwilini, mionzi hutumika kupunguza maumivu makali ya mifupa.
Madhara anayoweza kupata mgonjwa kutokana na aina hii ya tiba ni pamoja na kushindwa kusimamisha uume au uhanithi, kukosa hamu ya kula, uchovu, ngozi kubabuka, kuharisha na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
Tiba ya Homoni
Hii ni aina ya tiba inayotumia dawa zinazopunguza kiwango au ufanyakazi wa homoni ya testosterone mwilini. Testosterone ni homoni ya kiume inayochochea ukuaji wa tezi dume, hivyo basi matumizi ya dawa hizi husaidia kupunguza ukuaji huu na kusambaa kwa seli za saratani.
Tiba ya homoni hutolewa kwa wanaume walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu kwa nia ya kupunguza maumivu na kutibu dalili za ugonjwa. Dawa zinazotumika kwa tiba ya aina hii zimegawanyika katika makundi mawili, zile zinazochagiza uzalishaji wa homoni ya luteinizing (luteinizing hormone-releasing hormones, LH-RH) kwa mfano goserelin, nafarelin na leprolide; na zile zinazozuia ufanyaji kazi wa homoni ya androgen kwa mfano flutamide, bicalutamide na nilutamide.
Madhara yanayoweza kusababishwa na utumiaji wa dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu na kutapika, upungufu wa damu, kuongezeka uzito, uhanithi na kukosa hamu ya tendo la ngono, matatizo katika ini na matiti kuwa makubwa.
Baadhi ya madaktari hutumia upasuaji wa kuondoa korodani kama njia ya kupunguza kiwango cha homoni za kiume mwilini kwa kigezo kwamba kiwango kikubwa cha homoni hizi huzalishwa kwenye korodani. Hata hivyo tiba hii haifanyiki mara kwa mara.
Baada ya matibabu?
Baada ya matibabu, mgonjwa wa saratani ya tezi dume hufuatiliwa kwa ukaribu kuhakikisha kuwa saratani haisambai sehemu nyingine za mwili. Ufuatiliaji hujumuisha mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara pamoja na kupima PSA kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu mpaka mwaka mmoja.
Imeandikwa na Dr Fabian P. Mghanga
Daktari bingwa na Mhadhiri katika kitivo cha Afya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Jacob, Songea