Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 11:24 am

TUME YA UCHAGUZI KENYA: KILA KITU KIPO TAYARI KWA UCHAGUZI

Nairobi. Ikiwa imesalia siku moja tu kufikia siku ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo, IEBC imesema imekamilisha maandalizi yote ili wapiga kura waweze kutimiza haki yao ya katiba ya kumshagua viongozi wao.

IEBC iliyaeleza hayo mapema leo Jumatatu kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya walipokuwa wakielezea mfumo mzima wa kupiga kura. Vituo vyote 46,000 zitafunguliwa alfajiri ili wakenya milioni 22.1 wapige kura kutwa nzima hadi jioni.

Imearifiwa kuwa mchakato huo utamchukua mpiga kura dakika tatu kuitimiza haki yake endapo hahitaji usaidizi wa aina yoyote. Kila mpiga kura atapewa karatasi sita za rangi tofauti kuwachagua rais, gavana, seneta, mwakilishi wa wanawake, mbunge na mwakilishi wa wadi.

Vifaa vyote muhimu vimefikishwa vituoni

Mashine 55,000 za kielektroniki za kuwatambua wapiga kura zitatumika. Kila wadi itapewa mashini 6 za ziada kutumika endapo hitilafu yoyote inatokea. Ijapokuwa mfumo wa kuwatambua wapiga kura ni wa dijitali, daftari asilia litatumika pia kama ilivyoamuru mahakama kuu hasa katika maeneo yasiyokuwa na huduma za mtandao wa 3G.

Wafungwa pia wataweza kupiga kura ila kumchagua rais pekee. Jumla ya wafungwa 10,000 wamesajiliwa kupiga kura mwaka huu. Kwa atakayeharibu karatasi za kupigia kura, maafisa wa tume ya uchaguzi watakuwa vituoni kutoa usaidizi.

Kwa mujibu wa tume ya IEBC, waangalizi 10,000 wanashiriki kwenye mchakato wa uchaguzi huu. Asilimia kumi (10%) ya waangalizi hao wanatokea mataifa ya kigeni na wengine ni Wakenya. Ujumbe wa IGAD ulizinduliwa siku ya Jumapili baada ya kuhitimisha mafunzo. Rais wa zamani wa Ethiopia Mulatu Teshome ndiye anayeuongoza ujumbe huo.

IGAD ina wajumbe 24 wanaotokea mataifa 6 wanachama na watakuwa kwenye kaunti 10.Matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa kabla tarehe 16.