Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 10:07 am

NEWS: TANROADS KUTENGENEZA BARABARA KUU 36,362.

DODOMA: Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetaja vipaumbele vyake ambapo ni pamoja na kuratibu na kusimamia, ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na za mikoa zenye urefu wa kilometa 36,362.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 29,2022 jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mhandisi Mativila amesema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu mtandao wa barabara zenye lami ulikuwa umefikia kilometa 11,513.

“TANROADS inaendelea kudhibiti uzito wa magari barabarani na kulinda maeneo ya hifadhi ya barabara ambapo hadi sasa ina mizani 70 ya kudumu 22, ya kuhamishika mizani 15,”amesema Mhandisi Mativila

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya mendeleo amesema wamefanikiwa kukamilisha jumla ya miradi 14 yenye urefu wa kilometa 883 katika kipindi cha wa awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wenye gharama ya sh.Trilioni 1.37.

Mhandisi.Mativila ametaja miradi hiyo kuwa ni barabara ya Kidahwe hadi Kasulu yenye urefu wa kilometa 63, barabara ya Nyakanazi hadi Kibondo kilometa 50, Mbinga hadi Mbamba Bay kilometa 66, Njombe hadi Moronga kilometa 53.9, Moronga hadi Makete kilometa 53.30.

Ametaja barabara nyingine zilizokamilika kuwa ni ya Makutano hadi Natta kilometa 50 Mkoa, Kikusya Ipinda Matema kilometa 39.10 Chunya Makongolosi Kilometa 39.

“Miradi ya madaraja makubwa manne iliyokamilika ni pamoja na daraja la Tanzanite, Ruhuhu, Magara, Mara,Msingi,Singida ,Sibiti na daraja la Wami,

“Miradi mitatu ya madaraja makubwa ipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji kwa gharama ya Sh.bilioni 701 miradi hiyo ni daraja la J. P. Magufuli Kigongo Busisi km 3.2 (Mwanza) ,Pangani (m 520) Kitengule (m 140).

Aidha amesema kuwa serikali imekamilisha usanifu wa kina wa madaraja makubwa sita ambayo yanasubiri kuanza utekelezaji wake.

Madaraja hayo ni pamoja na daraja la Simiyu katika barabara ya Mwanza Musoma, Bwawa la Mtera katika barabara ya Iringa Dodoma, daraja la Mzinga katika barabara ya Dar es Salaam Kibiti, Mitomoni Ruvuma Mkenda Ruvuma na daraja la Jangwani.

Vilevile Mhandisi.Mativila amesema kuwa jumla ya miradi 44 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,523 yenye gharama ya Shilingi Trilioni 3.8 ipo katika hatua mbali mbali ya ujenzi nchi nzima.

“Miradi hii inahusisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani na inayogharamiwa kupitia Washirika mbalimbali wa Maendeleo,

“Aidha, mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 360,”amesema.

Pia Mha.Mativila ameeleza kuwa Miradi ya barabara 62 iko katika hatua mbalimbali za manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

“Barabara hizi zinajumuisha miradi inayogharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani pamoja na fedha kutoka kwa Washirika wa maendeleo,”amesema.

Aidha,amesema kuwa Miradi ya Madaraja Makubwa mitatu (3) ambayo ujenzi unaendelea ipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji kwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 701.

Miradi mingine ya Madaraja Makubwa sita ambayo usanifu wa kina umekamilika ambayo ni Simiyu (barabara ya Mwanza – Musoma), Bwawa la Mtera (barabara ya Iringa – Dodoma), Mzinga (barabara ya Dar es Salaam – Kibiti), Mitomoni (Ruvuma),na Daraja la Jangwani.

Ametaja miradi mingine kuwa ni Miradi ya EPC+ F ambayo Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imeanza utekelezaji wa Miradi ya EPC + F yenye urefu wa kilometa 2,533km. Makampuni yaliyokuwa “shortlisted’ yamealikwa tarehe 22 Septemba, 2022 kuwasilisha zabuni tarehe 22 Novemba, 2022.

“Miradi hiyo ni Kibaha – Mlandizi Chalinze – Morogoro (km 205) Expressway, Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (km 512),Arusha – Kibaya – Kongwa Road (km 493), Handeni – Kiberashi – Kijingu – Njoro – Olboroti – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambolo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 460), Igawa – Songwe – Tunduma (km 218), Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175),Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (km 389) na Mafinga – Mtwango (Km 81)

Mhandisi.Mativila pia ametaja Jumla ya miradi 43 ya barabara yenye urefu wa kilometa 2,021.04 na gharama ya Shilingi Bilioni 9.6 ipo katika hatua mbali mbali za upembuzi yakinifu na usanifu.

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, kati ya Julai 2021 hadi Mei 2022, jumla ya mikataba 20 inayohusisha miradi ya ujenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege inayogharimiwa moja kwa moja na fedha za ndani na mingine kugharimiwa kwa fedha za Washirika wa Maendeleo ilisainiwa,

“Mikataba ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya km 582.455 imesainiwa na mikataba ya ujenzi wa Kiwanja cha ndege Msalato na kumalizia jengo la Kiwanja cha ndege Songwe pamoja na mizani ya Rubana ilisainiwa na gharama ya miradi yote 20 ni Shilingi Bilioni 1,460.84

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Zamaradi Kawawa amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi katika kuboresha sekta ya Miundombinu kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),ilivyoelekeza.