Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 1:29 pm

NEWS: SEREKALI KULIFUTA DARASA LA SABA

Dar es salaam(na MuakilishiTZ). Serekali imesema kuwa imedhamiria kuondoa darasa la Saba hivi karibu hivyo Elimu ya Msingi nchini Tanzania itakomea Darasa la sita na hakutakuwa na mitihani ya taifa kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha tatu.

Kauli hiyo ya Serekali imetolewa hii leo Alhamisi na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Omary Kipanga katika uzinduzi wa kongamano la saba la kimataifa la uhandisi mitambo na viwanda uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Oktoba 20,2022

Kipanga amesea kuwa kufikia mwezi Disemba mwaka huu 2022 wizara ya elimu itazindua sera mpya ya elimu ili kuleta mabadiliko ya kielimu nchini.

Naibu Waziri wa Elimu Omary Juma Kipanga anaweka bayana kuwa ili kuwa na wahitimu wenye maatifa zaidi wizara yake imeanza kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa wizara hiyo Aprili 22, 2021, Bungeni Dodoma ya kutaka ifanye mabadiliko ya sera, mitaala na sheria ya elimu.

"Katika sheria na sera hii ijayo, elimu ya msingi itaishia darasa la 6 na hakutakuwa na mtihani wa Taifa bali tutakuwa na course assessment, baada ya kufaulu mwanafunzi atajiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo atakuwa tayari na mchepuo rasmi, kama ni kilimo ni kilimo, hakuna kusoma vitu vyote na tutakuwa na michepuo karibu 15 hivi, tunalenga huyu kijana akihitimu kidato cha 4 awe na uwezo wa kuwa na maarifa fulani na ujuzi ili aajirike au aajiriwe kama hatakwenda kidato cha 5," amesema Naibu Waziri Kipanga

Aidha Naibu Waziri Kipanga ameongeza, "Kuna mtazamo ambao mimi ninasema kwamba ndio uhalisia, wahitimu wengi hawaajiriki na hawana maarifa ya kujiajiri, hii ni changamoto sasa, sisi kama Wizara husika, tulipokea maelekezo ya Rais Samia alipohutubia Bunge Aprili 22, 2021, alitutaka tufanye mabadiliko ya sera, sheria na mitaala ya elimu yetu, sasa kufikia mwezi Desemba mwaka huu lazima tutazindua sera mpya ya elimu kwa lengo la kuleta mabadiliko kwenye mfumo wa elimu yetu na wataalam wetu na hapa tutaanza na elimu ya msingi hadi vyuo vikuu".

Katika hatua nyingine, Prof. Bakari Mnyiwiwa Rasi wa ndaki ya Teknolojia ya Uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anabainisha changamoto inayosababisha baadhi ya wahitimu kutokuwa wazuri katika maeneo ya kazi.

"Unajua tunaweza tukawa tunawalaumu wahitimu kwamba hawaajiriki lakini kumbe shida siyo wao, mhitimu wa shahada ya uhandisi kwa mfano anatakiwa apate hata mwaka mmoja wa kufanya kazi kiwandani chini ya usimamizi wa Mhandisi Mkuu au Kiongozi ambaye atakuwa na kazi ya kumuelekeza yule mhitimu nini kinafanyika huko, sasa wamiliki wengi wa viwanda sasa hivi hawapokei vijana wengi, lakini pia changamoto ipo kwenye kujikimu, huyu mhitimu atafanya kazi kwenye kiwanda bilà kupata chochote ataishije, kama kungekuwa na posho angalau ya kumfanya aishi basi wapewe nafasi kwenye viwanda ili wajifunze, wafanye uhandisi kwa vitendo sasa, na wakitoka hapo waajiriwe na hapo watakuwa na ujuzi wa hali ya juu, ndivyo tulikuwa tukifanya kipindi hicho viwanda vyote ni vya serikali," amesema Profesa Bakari Mnyiwiwa, ambaye Rasi ndaki ya Teknolojia ya Uhandisi, UDSM.

Kongamano hili litakalodumu hadi kesho Oktoba 21, litajadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kufikia agenda ya viwanda ya Tanzania pamoja na namna ya kukuza uzalishaji wa bidhaa za viwandani