Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 3:53 pm

NEWS: NFRA YASHUSHA NEEMA KWA HALMASHAURI 9 NCHINI.

DODOMA: Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) imesema imeanza kupeleka chakula cha bei rahisi katika halmashauri tisa nchini zenye mfumuko mkubwa wa bei za vyakula.



Akizungumza Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) CPA.Milton Lupa, wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Oktoba 2,2022 jijini Dodoma amesema ili kukabiliana na makali ya mfumuko wa bei za nafaka Wakala kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko ili kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

”Wakala unahudumia Halmashauri za Bunda, Sengerema, Geita, Nzega, Liwale, Nachingwea, Longido, Loliondo na Monduli ambapo takriban tani 3,000 zimepelekwa katika maeneo hayo.”amesema CPA.Lupa

Aidha amesema kuwa Wakala imejipanga kuhudumia maeneo mengine yatakayothibitika kuwa na mahitaji ya dharura au upungufu wa Chakula.

Ameeleza kuwa wakala unatekeleza Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka ambapo mradi huo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

CPA.Lupa amesema kuwa NFRA imefanikiwa kukamilisha sehemu ya Mradi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 90,000 katika kanda za Arusha (Halmashauri ya Babati) na Sumbawanga na Mpanda.

“Kukamilika kwa Mradi huo kumeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 341,000 na utekelezaji wa Mradi katika maeneo mengine Dodoma, Songea,Shinyanga,Songwe na Makambako umefika asilimia 85,”Amesema CPA. Lupa.

Kwa upande wa Ajira NFRA imefanikiwa kutoa ajira za muda mfupi kwa wananchi zaidi ya 3,000 zinazochangia kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Ajira hizo zinatokana na kazi mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi la ununuzi wa nafaka,uhifadhi na kipindi cha uzungushaji wa nafaka na utekelezaji wa Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka,”amesema

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kujihakikishia usalama wa chakula kuanzia ngazi ya Kaya,wahifadhi akiba ya kutosha ya chakula kipindi cha mavuno na kuuza chakula pale wanapokuwa na ziada katika uzalishaji.