Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 9:09 am

NEWS: NECTA YAFUNGIA SHULE 24 KUFANYA TENA MITIHANI

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limezifungia shule 24 kuendelea kuwa vituo vya kufanyia mitihani ya Taifa mara baada ya kugundulika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Shule hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani nchini, ndani yake zipo shule maarufu ikiwemo ya Musabe ya jijini Mwanza na St Anne Marie ya jijini Dar es Salaam na shule ya Rweikiza ya mkoani Kagera.

Uwamuzi wa kuzifungia shule hizo umeelezwa leo Desemba Mosi na Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2022.

Akizitaja shule hizo ni Kadama shule ya msingi iliyopo Chato- Geita, Rweikiza (Bukoba), Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), Al-hikma (Dar es Salaam).

Nyingine ni Kazoba (Kagera), Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani).

Pia zipo shule za Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza) na St Severine (Kagera).

“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” amesema.

Mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi ulihusisha watahiniwa zaidi ya 1.38 milioni nchi nzima.