Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 12:11 pm

NEWS: MFALME CHARLES III ATANGAZWA KUWA MFALME

Hatimaye mtoto wa Malikia Elizabeth II Mfalme Charles III ametangazwa rasmi kuwa mfalme wa Uingereza katika hafla ya kihistoria iliyofanyika kwenye kasri la Mtakatifu James, jijini London.

Baraza la Viongozi lenye jukumu la kumtangaza mfalme, lilimtangaza rasmi Mfalme Charles III siku ya Jumamosi na hafla hiyo imeoneshwa moja kwa moja katika televisheni ikiwa ni kwa mara ya kwanza. Baraza hilo linaundwa na wanasiasa wa ngazi ya juu na maafisa ambao wanamshauri mfalme.

Baraza hilo lilikutana kabla, bila ya Charles kuwepo wakati linatangaza rasmi jina la mfalme mpya kama mkuu wa nchi kuwa ni Mfalme Charles III.

Charles, mwenye umri wa miaka 73, mtoto mkubwa wa Malkia Elizabeth II alichukua kiti cha ufalme moja kwa moja mara tu baada ya kifo cha mama yake Malkia Elizabeth II, kilichotokea Septemba 8, na hafla ya kutangazwa rasmi Jumamosi ni hatua muhimu ya kikatiba na uthibitisho wa utambulisho wake kama mfalme mpya wa Uingereza.

Baada ya kutangazwa rasmi, Mfalme Charles III, aliungana na wajumbe wa baraza hilo na kula viapo kadhaa na kukiri matamko. Baada ya hapo Mfalme Charles III alitangaza rasmi kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth wa Pili, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96.


Katika hotuba yake Mfalme Charles III aliushuruku umma kwa kuwa pamoja na familia yake yote baada ya msiba huo. Amesema anafahamu kwa kina "majukumu mazito" ambayo amepewa kama mtawala mpya.

Mfalme asema ataiga mfano wa mama yake

"Katika kuchukua majukumu hayo nitajitahidi kuiga mfano wa kutia moyo wa mama yangu katika kufuata na kudumisha katiba na kutafuta amani, maelewano na ustawi wa watu wa visiwa hivi, na ulimwengu wa jumuia ya madola duniani kote," alisema Mfalme Charles III.

Pia alimshuruku mkewe, Camilla kwa msaada ambao amekuwa akimpa mara kwa mara. Kama ilivyo utamaduni, Mfalme Charles III pia alikula kiapo cha kudumisha usalama wa Kanisa la Scotland.

Mfalme Charles III alisindikizwa katika hafla hiyo na mkewe, Camilla pamoja na mtoto wake mkubwa Mwanamfalme William. William sasa ndiye mrithi wa kiti cha ufalme na anajulikana kama Mwanamfalme wa Wales, cheo ambacho kimekuwa kikishikiliwa na Charles kwa takribani miongo mitano.

Hii ni mara ya kwanza hafla hiyo inafanyika tangu mwaka 1952, wakati Malkia Elizabeth II alipotangazwa kuwa malkia wa Uingereza.