Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 8:34 am

NEWS: MAAGIZO YA BARAZA LA MAWAZIRI KUHUSU AJALI YA PRECISION

Dar es Salaam. Serekali ya Tanzania kupitia Baraza la Mawaziri nchini Tanzania, lililoketi hii leo Jumatatu chini ya Rais Samaia limeagiza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 wakinusurika.

Akizungumza leo Jumatatu Novemba 14, 2022 baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Baraza hilo limetoa maagizo ili kupata chanzo cha ajali na mapendekezo.

“Baraza la Mawaziri limewaelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi wa ajali hii na pia kupata chanzo cha ajali pamoja na mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa mara baada ya ajali kutokea” amesema

Amsema Baraza hilo limetoa maelekezo hayo kwa kuzingatia nchi imeingia kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa baada ya ajali kutokea.

“Ni muendelezo wa kutekeleza makubaliano hayo ndiyo maana Baraza limeelekeza wataalamu wetu wa nadani washirikiane na wataalamu kutoka nje na uchunguzi huu umeshaanza,” amesema

Msigwa amesema Baraza hilo pia limeelekeza 'Vitengo vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe mambo mbalimbali ambayo yatatuwezesha kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulionao sasa katika kukabiliana na majanga yanapotokea” amesema

Amesema baada ya ajali hiyo kutokea kuna hatua tatu ambazo zinafwatwa kwenye uchunguzi.

Msigwa amezitaja hatua hizo ni pamoja na timu ya uchunguzi ambayo inafanya uchunguzi na kutoa maelezo yake ndani ya siku 14, ikifuatiwa na ripoti ya awali ambayo inatolewa ndani ya siku 30 na hatimaye inatolewa ripoti kamili ambayo inatolewa ndani ya miezi 12.

Msigwa amesema hatua zote tatu zimeshaanza kufanyika na Serikali inawaomba wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi unafanyika.

Ndege hiyo ilianguka katika Ziwa Victoria takribani mita 100 kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mkoani Kagera ikiwa na watu 43 waliokuwa wakitoa jijini Dar es Salaam, kati yao 39 wakiwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili.

Baada ya ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, mwaka huu saa 2:53 asubuhi, shughuli za uokoaji kwa sehemu kubwa zilifanywa na wavuvi wakiongozwa na kijana Jackson Majaliwa na wenzake waliowezesha watu 24 kuokolewa.

Wakati Baraza hilo likitoa maelekezo kwa wataalamu, Kampuni ya Precision Air limesema tayari limeanza mchakato wa malipo ya fidia kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Patrick Mwanri amesema mchakato huo utakaokuwa kati ya familia za waliothirika na shirika hilo utakuwa wa siri na utafanyika kwa umakini mkubwa.

Ingawa Mkurugenzi huyo hakuweka wazi kiasi gani ambacho waathirika watalipwa lakini wiki iliyopita Mwenyekiti wa Chama cha Kampuni za Bima, Khamis Suleiman aliiambia Mwananchi kuwa inapotokea ajali ya ndege bima inatakiwa kumlipa mwathirika zaidi ya Sh300 milioni.