Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 2:55 pm

NEWS: KENYATTA KUONGEZA MUDA MADARAKANI

Nairobi MuakilishiTZ). Kesi za kupinga ushindi wa Rais Mteule William Ruto zilizowasilishwa katika Mahakama ya Juu nchini Kenya juzi Jumatatu wiki hii zimemwongezea Rais Uhuru Kenyatta muda wa kusalia mamlakani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya Rais Kenyatta anatakiwa kuondoka Mamlakani hapo siku ya Jumanne ya wiki ijayo ya Agosti 30, 2022.

Hatuo hiyo ya kukabidhi Ikulu imesogezwa mbele baada ya Mgombea wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na walalamishi wengine kwenda Mahakama ya Upeo kupinga matokeo yaliyotangazwa wiki iliyopita na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), inampa Rais Kenyatta muda zaidi kukaa Ikulu.

Majaji saba wa Mahakama ya Juu – Jaji Mkuu Martha Koome, Philomena Mwilu, William Ouko, Mohammed Ibrahim, Dkt Smokin Wanjala, Njoki Ndungu na Isaac Lenaola wanatarajiwa kutoa uamuzi wao Septemba 5, 2022.

Iwapo majaji hao wataamua kuwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 uliendeshwa kwa njia huru na haki kwa kuzingatia Katiba na sheria zilizopo, Rais Mteule Ruto ataapishwa Septemba 12, 2022.

Lakini Rais Kenyatta atasalia Ikulu kwa zaidi ya miezi miwili zaidi iwapo mahakama itabatilisha ushindi wa Dkt Ruto na kuagiza IEBC kuandaa uchaguzi mpya wa urais ndani ya siku 60.

Hilo likifanyika, IEBC itatakiwa kuandaa uchaguzi kati ya Septemba 13 na Novemba 13, 2022.

Wakili Dkt Erick Komolo anasema iwapo Mahakama ya Upeo itakubali ombi la Bw Odinga kutaka Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati atimuliwe na kuzuiliwa kushikilia wadhifa katika afisi ya umma, kutakuwa na utata ambao utaathiri uchaguzi mpya.

“Iwapo Mahakama ya Upeo itabatilisha ushindi wa Dkt Ruto, mrengo wa Bw Odinga hautakubali uchaguzi wa marudio kusimamiwa na Bw Chebukati. Itabidi Bw Chebukati ajiuzulu au achukue likizo ya mwisho akingojea kustaafu. Iwapo atajiuzulu Naibu Mwenyekiti Bi Juliana Cherera atajitwika jukumu la kuandaa uchaguzi. Kambi ya Dkt Ruto pia huenda isikubali Bi Cherera kutokana na imani kwamba anaegemea upande wa Azimio,” anasema Dkt Komolo.

Kifungu cha 7A (4) kinaruhusu Bi Cherera kutekeleza majukumu na mamlaka ya mwenyekiti iwapo wadhifa huo utakuwa wazi.

Kuapishwa

Bw Chebukati anatarajiwa kustaafu Januari 20, 2023.

Lakini sheria inamruhusu kuchukua likizo ya mapema ya siku 60 akingojea kustaafu. Ikiwa Bw Chebukati ataamua kuchukua likizo ya mapema, ataondoka Novemba 2022.

Iwapo uchaguzi wa urais wa marudio utabatilishwa tena kutokana na maandalizi duni ya IEBC, Rais Kenyatta anaweza kusalia afisini hadi mwaka ujao wa 2023.

Lakini Bw Bob Mkangi, wakili wa masuala ya katiba, anasema kuwa itakuwa vigumu kwa Mahakama ya Upeo kubatilisha uchaguzi wa urais mara mbili.

“Japo Katiba inaruhusu kubatilisha uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu, itakuwa vigumu kwa mahakama hiyo kubatilisha uchaguzi zaidi ya mara moja. Hilo litawezekana tu endapo IEBC itakiuka kwa kiasi kikubwa sheria wakati wa uchaguzi,” anasema Bw Mkangi.

Kifungu cha 142 (1) cha Katiba kinasema kuwa rais aliye mamlakani ataondoka tu iwapo mrithi wake ataapishwa.

Hivyo, Rais Kenyatta ataendelea kuwa Ikulu hadi pale mrithi wake ataapishwa.

“Rais atakuwa mamlakani kuanzia siku anayoapishwa kushikilia hatamu ya uongozi hadi pale rais mpya atakapoapishwa,” inasema Katiba.