Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 9:23 am

NEWS: IKUNGI YAMETIMIA, STENDI YA KISASA KUJENGWA.

DODOMA: Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu ameihoji serikali ni lini itajenga stendi ya kisasa Ikungi kutokana na umuhimu wa stendi hiyo ambayo inapokea magari mengi yanayopita yakielekea Mwanza na Dar es salaam.

Akijibu swali hilo Februari 2,2023,bungeni Jijini Dodoma, Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dkt Festo Dugange amesema halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika mwaka wa fedha wa 2022/2023,imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 110 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo.

“Serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri imekwisha lipa fidia kiasi cha Shilingi Milioni 36 ya eneo la ukubwa wa hekari 5 lililopo katika kijiji cha muungano Kata ya Unyahati ili kupisha ujenzi wa stendi hiyo,”amesema.

Katika swali la nyongeza Mtaturu ametaka kujua hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kuanza ujenzi huo mapema.

“Pia fedha zilizotengwa ni kidogo nini mkakati wa serikali wa kuongeza fedha ili kujenga stendi kubwa yenye hadhi kwa kuwa eneo hilo ni barabara kubwa inayopokea magari mengi yanayotoka Dar es salaam na Mwanza,”amehoji Mtaturu.

Akijibu maswali hayo,Dkt Dugange amesema halmashauri ya Wilaya ya Ikungi inauhitaji wa stendi ya mabasi yenye ubora itakayowezesha huduma bora za usafiri.

Amesema shughuli za awali za ujenzi zimeanza ili kuanza ujenzi huo huku tathmini iliyofanyika inaonesha zinahitajika sh.milioni 700 ili kukamilisha ujenzi wake.

“Tumekubaliana kupitia mapato ya halmashauri kila mwaka zitatengwa Sh.Milioni 150 na mwaka ujao wa fedha halmashauri imetenga fedha hiyo ili kuendelea na ujenzi,”amesema.