Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 9:38 pm

SPORT: BRAZILI KWA SASA NI MOTO WA KUOTEA MBALI

Timu ya Taifa ya Brazili jana imeishikisha adabu timu ya Taifa ya Austria kwa mabao 3 - 0 katika mechi yao ya mwisho ya kujiandaa na Kombe la Dunia mchezo uliopigwa mjini Vienna.

Wachezaji mastaa wa timu hiyo Gabriel Jesus, Neymar na Philippe Coutinho walifanikiwa kutikisa nyavu kila mmoja katika mchezo huo.

Mshambuliaji wa Manchester City Jesus alimpindua kipa Heinz Lindner kwa kombora la kujipinda na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 35.

Neymar, aliyekuwa ameanza mechi kwa mara ya kwanza tangu aumie Februari, aliongeza la pili katikati ya kipindi cha pili, baada ya kucheza kwa ubunifu mkubwa dakika ya 63.

Kiungo wa kati wa Barcelona Coutinho aliongeza la tatu muda mfupi baadaye kunako dakika ya 69.

Alifanikiwa kuukimbilia mpira uliokuwa umepenyezwa eneo la hatari na mwenzake wa zamani katika klabu ya Liverpool Roberto Firmino kabla ya kufunga.

Mambo yangekuwa mabaya zaidi kwa Austria, kwani Coutinho alitikiza mwamba wa goli dakika ya 76 naye Firmino akazuiwa kufunga na ustadi wa kipa dakika za mwisho mwisho.

Austria, walioshindwa kufuzu kwa michuano hiyo inayoanza Urusi baadaye wiki hii hawajacheza Kombe la Dunia tangu 1998.

Katika mechi hiyo, hawakutoa ushindani mkali sana kwa Brazil, ingawa mshambuliaji wa West Ham Marko Arnautovic alikaribia kufunga kipindi cha kwanza.

Brazil hawajashindwa hata mechi moja tangu Juni 2017, mechi 10.