Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 2:49 pm

RIPOTI: Mpaka sasa Rais Magufuli ametumbua zaidi ya watumishi 300

Dar es salaam: RAIS Dk. John Magufuli anaelekea kufunga mwaka huku akiwa amesafisha Serikali yake ya awamu ya tano kwa kuwatumbua watendaji zaidi ya 300 tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana


Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika uoza ndani ya Serikali, huku baadhi ya watendaji wa ngazi za juu wakihusishwa na tuhuma mbalimbali, ikiwamo za matumizi mabaya ya ofisi na ufisadi.

Hatua hiyo inaelezwa ni miongoni mwa mkakati wa kuzika mfumo wa Serikali ya awamu ya nne ambao baadhi ya vigogo walikuwa wakifanya mambo holela na kusahau wajibu wao kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Uchukuaji huo wa nidhamu kwa idadi kubwa ya watumishi wa Serikali, inaonyesha kuwa kila siku kuna wastani wa kigogo mmoja mtendaji wa juu ambaye amejikuta akifutwa kazi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutumia madaraka vibaya na kuisababishia hasara Serikali.

Fagio hilo linajumuisha watumishi wa Serikali waliosimamishwa kazi kutoka taasisi mbalimbali na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa.

Asilimia kubwa ya vigogo waliosimamishwa kazi walichukuliwa hatua na Rais mwenyewe na wengine Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, huku wawili wakiwajibishwa na mawaziri husika katika wizara wanazoongoza.

Tukio la hivi karibuni, kiongozi huyo wa nchi alitengeua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela, ambaye alitangaza utafiti wa ulioonyesha uwapo wa ugonjwa wa Zika nchini.

Dk. Mwele alisema utafiti huo ulifanywa na NIMR kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Bugando (Cuhas).

Siku moja baada ya kutenguliwa kwa kigogo huyo, Rais Magufuli alimtangaza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Yunis Mgaya kuwa mrithi wa nafasi hiyo.

WALIOTUMBULIWA

Wengine ambao waliondolewa kwenye nafasi zao na hata kujikuta wakifikishwa kortini ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake wanne.

Mbali na Maimu, wengine waliotumbuliwa ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa usafirishaji, George Ntalima.

Januari 15, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kufuta uteuzi wa aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk. Feisail Issa, ambaye ilidaiwa alitaka kupigana na Mkuu wa mkoa huo, Magesa Mulongo.

KIRANJA WA MAKATIBU WAKUU

Machi 6, mwaka huu Rais Magufuli, alitangaza kumng’oa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue kuhudumu katika wadhifa huo, Ikulu Dar es Salaam.

Balozi Sefue amehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 65 tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana.

Hatua hiyo ya kuondolewa katika nafasi hiyo ya kiranja wa makatibu wakuu wa wizara, ilikuja siku chache baada ya gazeti moja la wiki kuripoti juu ya kashfa na kumuhusisha Balozi Sefue na ufisadi katika miradi kadhaa ya maendeleo.

MA-RC

Machi 13, mwaka huu mkuu huyo wa nchi aliwaweka kando wakuu wa mikoa 13 baada ya kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo kati yao 13 ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa vituo vya kazi na mmoja alipangiwa Mkoa mpya wa Songwe.

WAZIRI MAMBO YA NDANI

Machi 20, mwaka huu Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Rais Magufuli alitengua uteuzi huo kutokana na kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu wizara yake akiwa amelewa.

Aprili 26, mwaka huu Rais Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk. Ally Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS) na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Machi 22, 2013 TCRA iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu. Kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano, lakini hadi wakti huo ilikuwa haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusu udhibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet).

source Mtanzania