Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 8:02 pm

Rais Mugabe kwenye Tuhuma tena, Atumia zaidi ya Bilioni 2 Kukodi ndege ya kifahari

Harare: RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe mwishoni mwa wiki iliyopita amefuja zaidi ya dola milioni moja za Marekani kwa ajili ya kukodi ndege ya kifahari Boeing 767-200 aliyoitumia kusafari katika nchi za Singapore na Ghana ilihali nchi yake ikikabiliwa na uchumi mgumu kupindukia.

Kwa mujibu wa Jarida la Indipendent, uchunguzi unabainisha kwamba ndege hiyo aliyotumia Rais Mugabe, 767 Boeing Business Jet (BBJ) yenye usajili P4-CLA, kuanzia Machi Mosi hadi Machi 6, mwaka huu, ilifanyiwa malipo katika kampuni yake ya zaidi ya dola za Marekani milioni moja. Ndege hiyo inaendeshwa na Kampuni ya Comlux Aviation, yenye ofisi zake Bahrain.

Inaelezwa kwamba ndege hiyo ya kifahari inavyo vyumba vya faragha, ofisi kubwa sambamba na muundo wa kuvutia ndani unaonakshiwa na vifaa vya kisasa.

Taarifa hizi za Mugabe kukodi ndege ya kifahari kwa fedha nyingi zinajitokeza huku tayari kukiwa kumeripotiwa taarifa nyingine zinazobainisha kwamba kiongozi huyo huyo amekuwa na matumizi ya ufujaji wa fedha katika usafiri.


Inadaiwa kwamba safari zake za ndani na nje ya nchi zimepata kutumia takriban dola za Marekani milioni 36 katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2016 katika nchi ambayo sekta ya afya imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa, zikiwamo hata dawa za kutuliza maumivu katika hospitali za umma.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Jarida la Independent, Mugabe amelazimika kukodi ndege hiyo ya kifahari baada ya ndege yake ambayo amekuwa akiitumia kwa safari zake ya Shirika la Ndege la Zimbabwe (AirZim) kuhitaji matengenezo makubwa kabla ya kuruka safari za masafa marefu. “Shirika la Ndege la Zimbabwe limeshindwa kuifanyia matengenezo yanayohitajika ndege ya Rais Mugabe kwa kuwa wakala wake wa vifaa bado hajalipwa deni lake la awali,” kilieleza chanzo cha habari cha Independent na kuongeza kuwa: “..shirika kwa sasa limekuwa katika hali mbaya.”