Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 2:42 pm

News: Yusuph Manji kuburuzwa kortini

Dar es salaam: MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Mehboob Manji, huenda akafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, kwa tuhuma za kughushi mkataba,

Vyanzo vya kuaminika vinadai kwamba jalada la kesi hiyo tayari limefika mezani kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, na wakati wowote suala hilo litafikishwa mahakamani.

Manji ambaye ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini Tanzania, anadaiwa kuwasilisha mahakamani mkataba ulioghushiwa wa upangaji katika jengo la PSPF Plaza, ambalo lilikuwa likijulikana kwa jina la Quality Plaza.

Mapema mwezi huu, kampuni zinazomilikiwa na familia ya Manji ziliamriwa na Mahakama ya Ardhi kutoka katika jengo hilo lililoko katika barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, baada ya kudaiwa kukaa bila kulipa kodi.

Kampuni hizo zilizokuwa chini ya Manji zilitakiwa ziwe zimehama kutoka katika jengo hilo kufikia Desemba 2 mwaka huu, baada ya kuwa zinadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 13 (dola milioni sita).

Baada ya Manji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu maarufu ya soka ya Yanga, kuwa amefukuzwa rasmi katika jengo hilo, gazeti hili limeambiwa kwamba sasa anaweza kufikishwa mahakamani kwa jambo jingine.

muandishi ameambiwa kwamba katika kesi hiyo inayotarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, PSPF inadai Manji alipeleka mahakamani mkataba ulioghushiwa ili aendelee kubaki katika jengo hilo.

Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za upangishaji wa jengo hilo la PSPF Plaza lililopo katika kitalu namba 189/2, Manji alianza kuwa mpangaji katika jengo hilo tangu mwaka 2005.

Kampuni za Manji ambazo zilikuwa ndani ya jengo hilo hadi Desemba 2, 2016 ni Quality Group Co. Ltd, Gaming Management Ltd, Q Consult Ltd na Quality Logistics Co Ltd.

Nyaraka hizo ambazo baadhi zinadaiwa pia zimepelekwa kwa DPP zinaeleza kwamba mgogoro wa upangaji ulianza dosari kuelekea mwaka 2010, ambapo Manji ndiye anadaiwa kuanza tabia ya kutolipa kodi ya jengo.

Baada ya kuona PSPF ikitaka kumfukuza kutoka PSPF Plaza, Manji alikwenda mahakamani kwa ajili ya kuweka zuio na inadaiwa kwamba hapo ndipo alipowasilisha mkataba huo unaodaiwa kuwa wa kughushi ili aendelee kubaki.

“Mimi nikwambie tu kwamba Manji sasa atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa. Uchunguzi ulikuwa unaendelea na ni matumaini yetu kwamba sasa atafikishwa mahakamani mwaka huu au mapema mwakani. Kila kitu kimekamilika,”


mmoja wa maofisa wa ngazi za juu katika ofisi ya DPP aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yake hakukiri wala kukana kuwepo kwa jalada la kesi ya Manji, lakini alisema watu wanapaswa kuacha ofisi hiyo iendeshe mambo yake bila shinikisho

“Hebu punguzeni presha jamani. DPP hawezi kupeleka mahakamani kesi ambayo haina sifa za kufikishwa mahakamani. Kama hilo jalada lipo na kila kitu kimekamilika, kesi itaenda tu. Lakini, kama kuna vitu bado havijakaa vizuri, DPP hawezi kuipeleka mahakamani. Sasa mimi siwezi kusema kama ipo au haipo lakini ninachojua mambo yakikamilika huwa hakuna kipingamizi,” alisema.

Gazeti La Raia Mwema awali limeambiwa kwamba jalada hilo lilifika mikononi mwa DPP mapema mwaka huu na kwamba karibu viongozi wote muhimu wa serikali sasa wanafahamu kuhusu jambo hilo.