Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 11:53 pm

News: Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi ataja sababu za ucheleweshwaji wa malipo ya watumishi wa kiwanda cha chai.

Dodoma: Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, imetaja kuwa ucheleweshaji wa malipo ya wakulima na wafanyakazi katika kiwanda cha Chai Maruku mkoani Kagera ulianza Septemba, 2011 kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Kagera Tea Company Ltd.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, William Ole Nasha alitoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba(CCM), Jasson Rweikiza.

Rweikiza ametaka kujua ni kwanini serikali haichukui hatua ya kuwasaidia wakulima na wafanyakazi ili wapate haki yao ambayo wamekuwa wakiitafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. “Kampuni ya Chai ya Maruku imekuwa sugu kwa kutowalipa wakulima wanaoiuzia chai pamoja na kutowalipa wafanyakazi wake wenyewe,”alisema Mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema kutolipwa kwa wakulima na wafanyakazi hao kulitokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Kagera Tea Ltd iliyowekwa na Spearshield Africa Company Ltd anayemiliki Kiwanda cha Chai cha Maruku.

Amebainisha kuwa anamiliki kwa asilimia 75 katika kusimamia uendeshaji wake ikiwemo ununuzi wa majani mabichi ya chai kutoka kwa wakulima wadogo huku wakulima hao wakimiliki asilimia 25 walizopewa na serikali kufuatia kiwanda hicho kubinafsishwa kwa Spearshield Africa Company.