- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
News: Waziri Maghembe kitanzini
Dar es salaam: WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amedaiwa kuongeza muda wa leseni za vitalu vya uwindaji kwa makampuni kinyume na taratibu za nchi.
Waziri huyo ameongeza muda wa uwindaji kwa wamiliki wa awali wa vitalu hivyo kwa muda wa miaka mitano; kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2022.
Katika barua pepe iliyotumwa kwa wanachama wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA) Januari 19 mwaka huu, wamiliki hao walitakiwa waende kwenye ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii kuchukua leseni zao zilizoongezewa muda.
Barua pepe hiyo ilieleza kwamba suala hilo la kuongezewa muda wa kutumika kwa leseni zao umefanikishwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa umoja wao huo.
" Kwa niaba ya Mwenyekiti wa TAHOA, Eric Pasanisi na Bodi ya TAHOA, napenda kuchukua nafasi hii kuwajulisha kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia juhudi kubwa za Eric, Mohamedtaki, Mike Angelides na Bodi ya TAHOA, imethibitisha kuongezewa muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji.
" Barua za kila kampuni kujua kama imeongezewa muda au la, kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Wanyamapori, zitakabidhiwa mkononi kwa mwakilishi wa kampuni atakayekwenda wizarani kuchukua barua hiyo, ilieleza sehemu ya barua pepe hiyo iliyoandikwa na Sheni Lalji," majira ya saa nane mchana, Januari 19 mwaka huu.
Hatua hiyo ya waziri Maghembe imepokewa kwa mshangao mkubwa na wadau wa sekta ya uwindaji kwa sababu imekuja kwa haraka na katika mazingira ambayo hayakutarajiwa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori namba tano ya mwaka 2009, utaratibu wa kugawa vitalu kwa ajili ya leseni una mtiririko wa taratibu ambazo waziri Maghembe hajazifuata.
Taratibu hizo zinahusu uwazi katika ugawaji wa vitalu hivyo, chombo cha kumshauri waziri katika kufikia uamuzi wa kugawa vitalu hivyo na suala zima la umiliki wa Watanzania katika sekta hiyo yenye kuingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ndicho kinachoweka utaratibu mwafaka wa kufuatwa kabla waziri hajatoa leseni upya kwa kampuni za uwindaji.
Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inataka kutangazwa kwenye magazeti utaratibu wa kuomba vitalu kwa waombaji katika kipindi kisichozidi siku thelathini (30) kuanzia tarehe ya tangazo.
Pia, inahitajika kufanyika kwa uchambuzi wa tathmini ya waombaji na kutangazwa kwa matokeo yake katika kipindi cha siku sitini (60) baada ya tarehe ya mwisho ya kupokea maombi.
Hata hivyo, vyanzo vya Habari vinaeleza kwamba waziri Maghembe hakufuata taratibu hizo zilizotajwa na badala yake ametumia madaraka aliyopewa kama waziri kuongeza muda wa leseni hizo.
Hata hivyo, madaraka ya waziri -kwa mujibu wa sheria hiyo, yanataka kufuatwa kwanza kwa taratibu nyingine; kama ya kushauriwa na chombo cha kumshauri waziri ambacho ndicho huzifanyia kampuni hizo tathmini.
" Kulikuwa na kamati ya kumshauri waziri huko nyuma lakini ya mwisho ilivunjwa na waziri Khamisi Kagasheki mwaka 2012 baada ya kuwepo utata kwenye ugawaji wa vitalu. Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, bila ya kamati hii, waziri kaongeza muda wa leseni za sasa kwa kutumia chombo kipi," alihoji mmoja wa wadau maarufu wa sekta hiyo.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu suala hili, waziri Maghembe alikana kukiuka taratibu zozote na kusema yote aliyoyafanya aliyafanya kwa mujibu wa sheria.
" Mimi nilichofanya kilikuwa ni kwa mujibu wa sheria. Hakuna jambo la ajabu. Mimi nikwambie kwamba hii wizara ina mambo mengi na ndiyo maana kila anayekuja hapa anaonekana mbaya.
" Nadhani tatizo langu ni kwamba nimekuwa mgumu katika kupindisha mambo na ninasimamia vizuri maslahi ya taifa. Wale waliozoea kupindisha mambo wanapata shida na hao ndiyo wanaopelaka maneno huku na kule,"