Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 11:46 am

NEWS: WAFANYABIASHARA WA MBAO WAMLILIA WAZIRI

DODOMA: Wafanyabiashara wa mbao nchini wamelalakimikia utitiri wa ushuru na tozo katika biashara hiyo ambapo wamedai kwamba umeua soko la mbao nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na Rais wa Shirikisho la viwanda vya misitu Tanzania (SHIVIMITA) Ben Sulus (kulia) wakati Rais huyo akiwasilisha taarifaya wamiliki wa viwanda vya mazao ya misituwakati wa kikao kilichofanyika jana mjini Dodoma,

Wakizungumza leo Mjini hapa katika kikao chao mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Josephat Hasunga, wafanyabiashara hao wamesema kwa sasa Tanzania ina tozo 32 na zote zinaingia kwa mlaji wa mwisho.

Mwenyekiti Mtendaji wa Mufindi Environmental Trust Dodfrey Mosha amesema kumekuwa na tatizo kubwa kwenye biashara hiyo na sasa wanashindwa kushindana na wenzao wa nchi zingine.


Mosha amesema kuwa katika masoko ya Dubai na Sudan hakuna Mtanzania anayefanya biashara huko ambaye anaweza kushindana na wenzao wa Chile na Finland.

"Hatukatai kodi Tatizo hapa kwetu mfanyabiashara amegeuzwa kuwa adui, kodi ni nyingi kiasi kwamba hatuwezi kufanya biashara ikatulipa licha ya mbao zetu kuwa bora zaidi ya wenzetu wengine," amesema Mosha

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu nchini(SHIVIMITA) Ben Sulus alisema hali ni mbaya kwa sasa katika biashara hiyo kutokana na serikali kupandisha bei za magogo na kushusha masoko ya ndani.



Sulus amelalamikia serikali kwamba imeshindwa kuwasaidia hata kuweka kitengo cha kushughulikia idara ya misitu ili kupata maoni ya wadau hao.

Akifanya majumuisho Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Josephat Hasunga amekiri kuwepo kwa utitiri wa tozo katika bidhaa za misitu akisema jambo hilo litaangaliwa.

Hasunga amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa serikali inapitia upya mifumo yote ili kubaini namna inavyowezakufanya ili kuwaondolea kero zitokanazo na misitu.

"Kwa utitiri huu hatuwezi kuwa na viwanda, hapa lazima tuunde chombo cha kusimamia suala la mazao ya misitu ambacho kitawasaidia kupunguza matatizo hating haraka," alisema Hasunga

Naibu Waziri aliwaondoa hofu kuhusu suala la mnada akisema serikali haitauza misitu yote kwa mnada badala yake uvunaji wa asilimia 30 ndiyo utakuwa mnada huku asilimia 70 itaendeshwa kwa njia ya makubaliano.

Kuhusina na suala la upandaji miti,Hasunga amesema linatakiwa kwenda kwa kasi zaidi ya uvunaji kwani Tanzania imekosa misitu ya uhakika wakati halmashauri za wilaya zimekuwa zikidanganya kwamba wanapanda miti 1.5 milioni kwa mwaka wakati si kweli.