Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 1:41 pm

NEWS: WABUNGE WAIVAA BODI YA MIKOPO, KUONGEZA VIGEZO VIPYA VYA MIKOPO

Dodoma: Wabunge wa bunge la Tanzania wamechachamalia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini juuu ya kuongeza vigezo vya kupata mikopo kila mwaka na hivyo kusababisha ugumu kwa watoto wa kimasikini kupata mikopo hiyo na kuitaka Serikali kupitia wizara ya Elimu kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo.

Wakiongea leo Mei 11, 2018 Wabunge ambao wameomba mwongozo Godluck Mlinga (Ulanga Mashariki-CCM), Julius Kalinga (Monduli-Chadema) na Kasuku Bilago (BuyunguChadema). Mlinga amesema jana bodi hiyo ilitangaza kuanza udahili wa wanafunzi wanaomba mikopo ya elimu ya juu lakini wakaweka sharti kuwa wanaoomba wazazi ama walezi wasiwe na leseni za biashara. “Mlianza na wanafunzi waliosoma private (shule binafsi), mkaja watoto wa wabunge, wakurugenzi, wakuu wa wilaya na maofisa tukanyamaza sasa mmekuja na wanaomiliki leseni za biashara,”amesema.

Amesema kuwa wamachinga sasa hivi ambao hawana leseni wameshaambiwa wapewe namba TIN na ni wazi baadaye watapewa leseni. Mlinga amesema kwa kuongeza masharti kila mwaka, bodi hiyo ina mkakati wa kuwafanya watu wote wanaoomba mkopo wasikidhi vigezo.

Kwa upande wake, Kalinga amesema bunge limepitisha sheria na kuna kanuni zinazoongoza bodi hiyo lakini kila mwaka kumekuwa na matamko yanayochochea kuwanyima mkopo watoto wa masikini. “Serikali itoe ufafanuzi kuhusu matamko hayo kwa kuhakikisha haki inapatikana, haibagui na inasimamiwa na sheria pamoja na Katiba,”amesema. Bilago amesema vigezo vya kupata mikopo vimekuwa vikiongezwa kila mwaka kuhakikisha kuwa wanawabana wanafunzi wasipate mikopo. “Kila kukicha wanaoongeza vigezo ni ubaguzi. Walisema kila anayeomba asiwe anajaza fomu za maadili, diwani anajaza fomu ya maadili hivi ana mshahara gani?” amehoji