Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 2:45 am

NEWS: SPIKA NDUGAI KUSHTAKIWA KWA KUVUNJA KATIBA

Shirika la Elimu ya Uraia na Msaada wa Sheria (CILAO),ambalo ni shirika mwanachama la Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDCOALITION) limeandaa azimio la kumshtaki Spika wa Bunge wa Tanzania Job Ndugai kwa ukiukwaji wa KATIBA.

Azimio hili limekuja siku chache baada ya Spika Ndugai kumrudisha aliyekuwa Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe kupitia chama cha Chadema kurudi Bungeni bila ya kuwa na Chama anachokiwakilisha.

Mwambe alijiuzulu nafasi zote ndani ya chama chake cha zamani Chadema Februari 15, 2020 kisha akajiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

"Shirika la CILAO limesikitishwa na kitendo cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai kufanya maamuzi yanayokiuka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," imesema sehemu ya azimio hilo.

Ibara ya 71 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuhusu ukomo wa mtu kuwa Mbunge.

Ibara hiyo ya 71(1)(e) inaeleza bayana kuwa Mbunge atapoteza nafasi yake ya ubunge ikiwa atapoteza uanachama wa chama chake kilichompatia dhamana ya ubunge wakati wa uchaguzi.


"Kwakuwa Mwambe alishatangaza kijiondoa Chadema, basi tunaamini pasipo shaka kwamba alipoteza tayari sifa ya kuendelea kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," linasema azimio hilo ambalo mpaka sasa limeshasainiwa na zaidi ya watu 1,500.