Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 1:39 am

NEWS: SHULE YA ST. FLORENCE YAMKIMBIA MKUU WA WILAYA ALLI HAPI

Dar es salaam: Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum ali Hapi amejikuta anakimbiwa na uwongozi wa Shule ya Msingi St Florence Academy iliyopo Mikocheni Jijini Dar es salaam wakati akitembelea shule hiyo ili kuongea na uongozi wa shule.

Mkuu wa wilaya huyo amewasili shuleni hapo kutokana na sakata la udhalilishaji wa wanafunzi wanne wa darasa la saba shuleni hapo unaodaiwa kufanywa na mwalimu anayetambulika Ayoub Mlubu.

Hapi aliwasili shuleni hapo saa 7;56 mchana, ambapo alikwenda moja kwa moja kwenye Ofisi ya Mkuu wa shule hiyo lakini hakukuta mtu na kuamua kwenda kwenye ofisi nyingine za walimu ili kuzungumza nao lakini walimu hao walimkimbia na kufunga mlango.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kuzunguka kwenye madarasa ya shule kuonana na uongozi wa shule lakini katika hali ya kushangaza walimu waliokua kwenye madarasa hayo walifunga milango jambo ambalo lilimfanya azunguke bila utaratibu.

Baada ya muda, Mkuu huyo wa Wilaya alionana na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Wilson Mwabuka ambaye alimchukua na kumpelekea Ofisi kwake kuzungumza nae.

Baadae kidogo walitoka na mwalimu hiyo na kuelekea kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Shule hiyo ambapo waliingia ndani kuzungumza na kuwazuia waandishi wasiingie ndani kwa muda.

Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Hapi alitoka nje na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kinachoendelea shuleni hapo.

“Nimekuja baada ya kupata taarifa kutoka kwa watu mbalimbali kuhusiana na Mwalimu anayedaiwa kuwabaka watoto, kitendo hicho ni kosa kisheria kwa sababu kinawanyanyasa watoto kingono na kuwanyima haki zao.

“Hivyo basi, namuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo kufuatilia suala hilo kwa undani pamoja na kuwahoji walimu, wanafunzi na watendaji wote wa shule hiyo ili kujua ukweli na upelelezi ukamilike mapema na mhusika ikiwa atabainika amefanya kosa hilo afikishwe mahakamani.

“Naomba niwatoe hofu wananchi wa Kinondoni kuwa suala hilo limefanywa na mtu mmoja si shule, hivyo walimu wengine au uongozi wa shule usihukumiwe kwa kosa la mtu mmoja itakua hatujawatendea haki, tuviachie vyombo vya ulinzi na Usalama viweze kufanya kazi yake,” amesema.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwabuka suala hilo liachiwe polisi wafanye kazi yao.