Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 6:15 pm

News: Sakata la Lissu lamfanya Mbowe kucharuka Dar

Dar es salaam: Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema anasikitishwa na vitendo vya kukamatwa wabunge wakiwa ndani ya vikao, huku Ofisi ya Bunge ikikaa kimya bila kutoa tamko.

akirudia tena kulizungumzia swala hilo leo baada ya kumtembelea tena Lissu leo, ambaye yuko mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, Mbowe alisema Ofisi ya Bunge inajua wabunge wana kinga ya kisheria, lakini wamekuwa hawachukui hatua wala kutoa kauli yoyote.

“Tunasikitishwa na vitendo vya kukamata wabunge wakiwa ndani ya vikao vya Bunge na hasa wabunge wa upinzani, wanaendelea kukamatwa wengine wanafungwa na wengine wanapotezewa muda wao wa Bunge.

“Wabunge wanakamatwa Dodoma wanasafirishwa usiku wa manane kama vibaka halafu wananyimwa dhamana, viongozi wa Bunge hawatoi kauli yoyote… haya mambo yanayotokea si ya kawaida,” alisema Mbowe.

Alisema Lissu amehojiwa kwa kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi, wakati akijadili suala la njaa katika Taifa.

“Sasa Lissu kama viongozi wengine wa Chadema, vyama vingine vya siasa na madhehebu mbalimbali ya dini, walitahadharisha hali ya kuwapo kwa njaa katika Taifa. Lakini ndani ya Bunge kauli ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa Kilimo ilithibitisha kwamba watu zaidi ya milioni 1.5 wanakabiliwa na njaa na karibu 200,000 wana shida kali ya njaa.

“Kauli alizoongea Lissu zimeshathibitika si za uongo na tunashangaa mwezi mmoja umepita na Serikali imeshatoa kauli ya kuthibitisha shutuma zilizotolewa na viongozi wa dini, kisiasa na hata wa kijamii, lakini bado wamemshika Lissu na wamekataa kumpa dhamana,” alisema.