Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 2:44 am

NEWS: NSSF YATANGAZA BEI YA KUPANGISHA NYUMBA ZAKE

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetangaza bei halisi ya nyumba zake ambazo zimepitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali, kwamba kodi ya nyumba ni kati ya Sh. 250,000 mpaka Sh. 500,000.

Kwa mujibu wa NSSF ni kwamba kutokana na kodi hiyo mteja anaweza kulipa kuanzia mwezi mmoja, miezi mitatu hadi mwaka kutegemeana na aina ya nyumba anayotaka kupangisha.

Akizungumza alipotembelea mradi wa nyumba Dungu uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio amesema kuwa kwenye mradi huo wa Dungu nyumba zilizokamilika ni 99, kati ya hizo 59 tayari zimepangishwa, nyumba 10 zimekabidhiwa Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kigamboni na nyumba 16 zimekabidhiwa wakuu wa idara za halmashauri ya Kigamboni. Zimebaki nyumba 15 tu.

"Mpangaji anatakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha pamoja na shilingi 100,000, kwa ajili ya Service charge," amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Miliki wa NSSF, Augustino Paul amewataka wananchi kuchangamkia nyumba zilizoko Kigamboni na Tuangoma ambazo bei zake ni nzuri kwenye kupangisha. Amesema NSSF ina nyumba 76 zilizoko Toangoma ambazo zinauzwa na kupangishwa kwa wananchi.

Pia ameongeza nyumba hizo zinapangishwa kati ya shilingi 350,000 na 400,000 kwa mwezi na kwamba Shirika pia lina nyumba 33 zilizopo Mtoni Kijichi ambazo nazo zinazopangishwa kati ya Sh. 400,000 hadi Sh.500,000.

Amefafanua kuwa nyumba zote ni za kisasa na zina huduma zote na kwamba wananchi wote wanakaribishwa kuchangamkia fursa hiyo.