- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: NEEMA YAWASHUKIA PACHA WA BUKOBA KUTENGANISHWA SAUDI ARABIA.
Serikali ya Saudi Arabia imesema itagharamia matibabu nchini humo kutenganisha pacha walioungana, Anisia na Almesia, wenye umri wa miezi mitano, yatakayofanyika nchini Saudi Arabia.
Watoto hao walizaliwa Januari 29, wilayani Misenyi katika Kituo cha Masista cha St. Theresa Omukajunguti Kata ya Kyaka na kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam mapema mwezi Februari, ambako wamewekwa kwenye wodi maalumu ya jengo la watoto ya Magufuli, wakipatiwa matibabu ya awali kabla ya kupelekwa Saudia Arabia kwa matibabu.
Watoto hao wa Jonisia wameungana eneo kubwa la kifua na tumbo, lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa.
Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al – Hazani amesema kuwa watoto hao watafanyiwa upasuaji huo wa kuwatenganisha katika Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical iliyopo Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, ambako kuna madaktari bingwa wa upasuaji.
Alisema mpango huo wa kufanikisha matibabu ya upasuaji wa kuwatenganisha mapacha hao, unafanywa kwa ushirikiano wa ubalozi wa Saudi Arabia nchini chini ya balozi wake Mohamed Bin Mansour, uongozi wa Hospitali ya Muhimbili na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga.
“Mara tu mipango na maandalizi itakapokamilika, tunatarajia watoto kuondoka kwenda Riyadh mwishoni mwa mwezi huu," alisema Al-Hazani.
Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical huko Riyadh, ina uwezo mkubwa ikiwa na vifaa vya kisasa na vitanda 1,501 na ilianza shughuli zake Mei 1983.
Tangu wakati huo, imeendelea kupanuka, huku ikitoa huduma kwa idadi ya wagonjwa wanaokua kwa kasi katika maeneo yote.
Mama wa pacha hao, Jonisia Jovitus (21) alisema tayari watoto wake wamechukuliwa vipimo mbalimbali na jopo la madaktari wa Hospitali ya Muhimbili na kuvituma Saudi Arabia.
"Madaktari wameniambia walishatuma vipimo Saudi Arabia na uwezekano wa watoto wangu kutenganishwa upo, naomba Mungu asaidie hili lifanikiwe… ila walichoniambia ni kuwa wanangu wakifanikiwa kutenganishwa salama watakuwa walemavu, mmoja atakuwa na mguu mmoja na mwingine ana miguu miwili, lakini huo mmoja hauna nguvu umepooza. Ninachoomba kwa sasa ni kuwaona watoto wangu wametenganishwa na kuwa salama, naomba jamii iniombee ili lifanikiwe.”- Jonisia
Uongozi wa Hospitali wa Muhimbili kupitia kwa Ofisa Uhusiano, Aminiel Eligaesha ulisema kuwa utaweka wazi kuhusu mchakato mzima wa watoto hao madaktari watakapokuwa tayari.
Awali, uongozi huo wa Muhimbili ulikuwa uzungumze na vyombo vya habari juzi, lakini waliahirisha kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika wamepata dharura, hivyo vyombo vya habari vitaarifiwa siku itakayoitishwa upya mkutano huo.
Credit: Habarileo