Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 7:49 pm

NEWS: MUHIMBILI YAONDOA UVIMBE KWENYE INI BILA KUFANYA UPASUAJI

Dar es salaam: Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imekuwa hospitali ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki baada ya kuanza kutoa huduma ya kuondoa uvimbe kwenye ini kwa kutumia utaalam wa kifaa cha hadubini bila kufanya upasuaji.

Hadubini ni kifaa muhimu cha sayansi kwa utafiti wa vitu ambavyo ni vidogo mno kuonekana kwa jicho la binadamu.Mkuu wa Kitengo cha Mfumo wa Magonjwa ya Chakula na Ini Idara ya Tiba kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dk. John Rwegasha, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa wameanza na wagonjwa 40 ambao watapata huduma mbalimbali za magonjwa kwa kutumia kifaa hicho.

Dk. Rwegasha alisema upo uvimbe ambao haufikiki kwa njia ya upasuaji au namna yoyote hivyo kwa hutumia utaalam wa hadubini hufikiwa kwa urahisi na mgonjwa kuhudumiwa siku hiyo hiyo na kuruhusiwa. “Ujuzi huu tulikuwa hatuna, lakini kwa kushirikiana na wenzetu kutoka India na Afrika Kusini wametusaidia vyombo ambavyo vinafanya hadubini ambavyo vinachunguza na kutibu bila mgonjwa kupasuliwa,” alisema. Dk. Rwegasha alisema Muhimbili imethubutu kutoa utaalam huo na inafanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na Kenya watafanya mwezi Agosti kwa ushirikiano na Marekani. “Tanzania tumethubutu na tayari vifaa vimeshaingia nchini.

Tuna idadi ya wagonjwa 20 wanaosubiri kupata huduma hizi ambazo tangu Jumatatu tumezianza na tunaendelea kutoa huduma za kongosho na ini kwa kutumia mfumo wa hadubini ya X-Ray,” alisema

Rwegasha alisema tayari wamewasaidia wagonjwa 25 ambao kimsingi ingekuwa zamani wangehitajika kwenda nje ya nchi kwa sababu ujuzi huo haukuwepo. “Tunaushukuru uongozi wa Muhimbili kwa kuwasafirisha hawa wataalam kutoka India na kuwaleta Tanzania ili kutujengea uwezo wa utaalam,” alisema. Dk. Rwegasha, alisema Muhimbili ilianza mkakati wa kuimarisha huduma zake za kibingwa na kwa sasa mchakato wa upandikizaji ini unaendelea. “Tumeshaboresha huduma za masikio, figo na mwezi Desemba mwaka jana tulituma timu ya wataalam kwenda India kupata utaalam wa upandikishaji wa ini katika magonjwa ya ini na kongosho,” alisema. Dk. Rwegasha alisema upandikizaji wa ini sio jambo ambalo linaweza kufanywa mara moja bali linahitaji miundombinu ikiwamo mifumo ya hadubini ya uchunguzi. “Upandikizaji wa ini ni shughuli pana zaidi ikilinganishwa na figo na huhitaji wataalum kujiandaa, maandalizi yanahitaji muda, kuna vitu vya msingi vinatakiwa kufanyika kabla ya shughuli za upandikizaji kuanza nchini,” alisema. Pia alisema kufanya upasuaji mmoja wa ini unahitaji chupa 20 za damu ziwe tayari kwa ajili ya dharura yoyote itakayotokea na gharama kwa mgonjwa mmoja ni dola za kimarekani 1000.

chanzo Nipashe