- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
News: Mawakili wa LEMA waanza kupata ushida ombe la kupewa dhamana Baada ya siku 50
ARUSHA: MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ameanza kuona dalili za kutoka mahabusu anakoshikiliwa kwa siku 50 sasa, baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, kukubali maombi ya mawakili wake ya kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa dhidi ya dhamana yake.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Dk. Modesta Opiyo, anayesikiliza shauri hilo, alitoa siku kumi kuanzia jana kwa upande wa mshtakiwa huyo, kuwasilisha maombi yake ya dhamana nje ya muda.
Awali upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi mbili katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, ukiiomba mahakama hiyo isisikilize maombi hayo kwani hayakufuata taratibu za kisheria.
Desemba 16 mwaka huu, Jaji Dk. Opiyo alitupilia mbali pingamizi hizo na kusema mahakama haioni sababu ya msingi ya kumnyima haki Lema kwa kuwa hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa wajibu maombi, hazikuwa na mashiko kisheria.
Akisoma uamuzi wake jana, Jaji Dk. Opiyo alisema busara ya mahakama iliyo na nia ya kuendelea kutoa haki, inakubali maombi na inampa mleta maombi siku 10 kuanzia jana ili awasilishe maombi yake nje ya muda.
Jaji Dk. Opiyo ambaye alianza kusoma uamuzi huo jana saa 6:26 mchana hadi saa 7:18, alisema kesi inapoondolewa mahakamani, haifungi milango ya kukata rufaa nyingine ambayo ni haki ya mtuhumiwa.
“Mahakama hii kwa kuzingatia uamuzi wa kesi mbalimbali, ni lazima izingatie na kuangalia sababu, muda na athari ambazo zitatokana na uamuzi wake.
“Mahakama haikubaliani na hoja za upande wa wajibu maombi na imeona ucheleweshwaji wa notisi ya kusudio la kukata rufaa ulikuwa na sababu za msingi, hivyo inakubali maombi haya na inampa mleta maombi siku kumi kuanzia sasa.
“Kwa kuzingatia haki, walichelewa kwa sababu za msingi, hivyo mahakama haijaona kuwa ucheleweshwaji huo ni wa makusudi na katika siku mbili au tatu walizochelewa, kulikuwa na mashauri mengine yaliyokuwa yakiendelea mahakamani,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
Katika maombi hayo, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili, Matenus Marandu na Hashimu Ngole, huku upande wa mleta maombi ambao wanamtetea Lema, unawakilishwa na mawakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.
Baada ya uamuzi huo, Lema alirudishwa mahabusu akisubiri hatima yake iwapo mahakama itampa dhamana au vinginevyo.
Wakizungumzia uamuzi huo, mawakili wa pande zote mbili walikubaliana na uamuzi wa mahakama hiyo. Wakili Ngole alisema hawana pingamizi lolote.
Naye Wakili Mfinanga alidai kuwa wameridhishwa na uamuzi wa mahakama na tayari wameanza mchakato wa kuwasilisha maombi ya rufaa ya mteja wao.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni, zinasema mawakili hao walifanikiwa kuwasilisha rufaa yao na kupewa namba 126 ingawa ilikuwa haijapangiwa jaji wa kuisikiliza.
Pamoja na hayo, leo Lema atafikishwa tena mahakamani katika kesi ya kutuma ujumbe wa matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Katika kesi hiyo, mkewe Lema aitwaye Neema Lema, naye ni mshtakiwa.
mtanzania