Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 6:03 pm

News: Mali za Kampuni ya Mo Dawji mbioni kupigwa MNADA

Dar es salaam: WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na manispaa za Jiji la Dar e s Salaam imetoa notisi kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi, ambao ni pamoja na Kampuni ya Mohammed Enterprises.

Kampuni ya Mohammed Enterprises inatajwa kudaiwa shilingi milioni 73 na imewekwa katika kundi moja la wadaiwa sugu na hoteli ya Lamada inayodaiwa shilingi milioni 54.

Hayo yamebainika leo, Februari 3, 2017 wakati wizara ikiwa katika mwanzo wa oparesheni maalumu ya kukusanya kodi ya pango la ardhi kutoka kwa wadaiwa sugu iwe ni kampuni, mashirika ya kiserikali na watu binafsi.

Mbali na Mohammed Enterprises na Hoteli ya Lamada, wadaiwa wengine sugu kwenye orodha hiyo ni pamoja na Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) inayodaiwa shilingi milioni 144 na Tanganyika Motors inayodaiwa shilingi milioni 22.

Kampuni na taasisi hizo zimepewa notisi ya siku 14 kulipa kodi hizo wanazodaiwa na endapo hawatalipa watafutiwa umiliki au mali zao kupigwa mnada ili kufidia gharama madeni hayo.

Operesheni hiyo imeanza kutekelezwa kwa mtindo wa aina yake ambapo wahusika hufuatwa kwenye ofisi zao. Operesheni hiyo inaendeshwa kwa kushirikisha kampuni ya udalali ya Msolopa Investment.

Akizungumzia operesheni hiyo mbele ya waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Yamungu Kayandabila alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wizara hiyo imepanga kukusanya shilingi bilioni 111.77 kutokana na kodi ya pango la ardhi.

“Wizara haitaweza kufanikisha malengo hayo endapo itaendelea kuwaachia wadaiwa sugu ambao hawataki kulipa kodi. Kwa miaka mingi sasa mapato mengi ya serikali yamekuwa yakiachwa kutokana na kushindwa kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi,” alisema Kayandabila