Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 3:47 pm

News: Maandamano yaendelea baada ya Askari wa Israeli aliyempiga risasi mpalestina kutiwa hatiani na mahakama

Tel Aviv: Mahakama ya kijeshi ya Israel imemtia hatiani askari wa nchi hiyo, Elor Azaria, kwa kuua kwa kutokusudia jana baada ya kumpiga risasi Mpalestina aliyekuwa amejeruhiwa baada ya kumshambulia askari mwingine wa Israeli kwa kisu.

Mamia ya waandamanaji waliokuwa wanamuunga mkono Azaria walikuwa nje ya mahakama huko Tel Aviv ambapo kesi hiyo ilikuwa ikiendelea, na wanasiasa maarufu wamekuwa wakitoa wito kwa askari huyo kupewa msamaha.

Lakini uongozi wa jeshi la Israeli ulisema kwamba utaheshimu hukumu itakayotolewa hata kama hautaipenda.

Sajini Azaria alikuwa akifanya kazi huko Hebron, eneo ambalo lina Wapalestina wengi huko Ukanda wa Magharibi, alipompiga risasi al-Sharif, ambaye alikuwa ni mtuhumiwa na shambulizi la kisu. Askari wa Israeli alipatwa majeraha kidogo.

Kulingana na Jeshi la Israel, IDF, Azaria alifika katika eneo la tukio dakika baada ya shambulizi, akaweka risasi moja kwenye bunduki yake na kumpiga risasi al-Sharif kichwani, na kumuua papo hapo.

Azaria alikana mashtaka dhidi yake.

Lakini majaji watatu waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo waliamua kwa kauli moja kumtia hatiani kwa kuua bila kukusudia na utovu wa nidhamu.

Kitovu cha kesi kilikuwa ni kitu kilichomhamasisha akari huyo kutenda hayo. Mawakili waliokuwa wanamtetea Azaria walisema kwamba alihisi kuwa maisha yake yalikuwa hatarini, wakati upande wa mashtaka ukatoa hoja kwamba alihamasishwa na uovu na kulipa kisasi.

Katika maelezo marefu kabla hukumu haijatolewa, majaji walipinga hoja zote za upande wa utetezi.


Jaji Kiongozi, Kanali Maya Heller, alisema kwamba Azaria hakuwa shahidi wa kuaminika na kwamba mashahidi wake wa kumtetea walikuwa na matatizo. Aliita tukio la kumpiga risasi Mpalestina huyo kuwa halikuwa linahitajika. Wanasheria wa Azaria wameahidi kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo