Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 6:58 pm

NEWS: LISSU KUINGIA NCHINI TAREHE 27 NA NDEGE YA ETHIOPIA

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu ameahidi kuwa wiki ijayo siku ya Julai 27, 2020, ataingia rasmi nchini Tanzania akitokea nchini Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mwaka 2017 jumbani kwake mjini Dodoma.

Lissu amesema atasafiri na shirika la ndege la Ethiopia majira ya saa saba mchana kupitia uwanja wa Mwalimu nyerere Jijini Dar es salaam.

Ratiba hiyo ya Lissu ameitoa hii leo Julai 21, 2020, wakati akizungumza mujo kwa moja kupitia channel ya Youtube ya chama hicho na kueleza kuwa licha ya kwamba ameamua kurudi nchini lakini bado yuko kwenye hatari zaidi kwa kuwa wale waliomshambulia na kumjeruhi bado hawajulikana hivyo anayo imani kwamba bado wapo.

"Baada ya miaka karibu mitatu ya matibabu, wakati wa mimi kurudi nyumbani umewadia, kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, 2017, nitakanyaga ardhi na udongo wa Tanzania siku ya Jumatatu, Julai 27, 2020, Mjini Dar es Salaam, majira ya saa 7:20 mchana na nitaingia na Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia"amesema Tundu Lissu.

Akizungumzia suala la usalama wake Lissu amesema, "Wale waliokuja kuniua miaka mitatu iliyopita na waliowatuma, bado wanaitwa watu wasiojulikana, maana yake ni kwamba bado wapo, na hawajasema kama lengo lao la kuniua wameliacha bado kuna hatari ya maisha yangu, ninarudi nchini katika mazingira ambayo hatari dhidi yangu haijaondoka bado, lakini narudi tu ni nyumbani kwetu".