Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 8:28 pm

News: LISSU aunyemelea Urais TLS

Dar es salaam: Mbunge na mwanasheria wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Tundu Lissu (49) anapewa nafasi kubwa ya kushinda nafasi ya Urais katika chama cha mawakili Tanzania (Tanganyika Law of Society ) amabacho kinatarajia kufanya uchaguzi wake Juma mosi hii March 18 Jijini Arusha, Lissu anapewa chepua na mawakili wengi vijana kwani inaonekana kuwa swala la Umri ni sehem ya vigezo vinavyo mfanya Lissu kuchaguliwa na mawakili wengi vijana ambao kimsingi ndio wapiga kura walio wengi katika chama hicho.

Zipo sababu kuu tatu ambazo zinazo mfanya Lissu kushinda kiti hicho Sababu hizo tatu zinazodaiwa kumbeba Lissu kwenye uchaguzi huo wa aina yake ni – dhamira ya wanachama wa TLS kuwa na chama kinachotimiza majukumu yake ipasavyo, idadi kubwa ya wapiga kura kuwa vijana ambao wanampenda Lissu na pia kutaka kuionyesha serikali kuwa chama hicho ni huru.

“ Sababu ya kwanza ni kwamba ingawa TLS ni mojawapo ya taasisi kongwe nchini, ikiwa imeanzishwa mwaka 1954, haijulikani sana miongoni mwa Watanzania.

“ Ni kama vile imelala. Lakini, kama umebaini, tangu ijulikane kwamba Lissu atawania nafasi hiyo, vyombo vya habari vinaandika na watu wanazidi kuifahamu. Tumepata picha kwamba kumbe taasisi yetu inamhitaji mtu wa aina yake,” alieleza mmoja wa wanasheria aliyezungumza na muandishi wetu kwa masharti ya kutotajwa jina.

Mahojiano mengine na mawakili kadhaa yameonyesha pia kwamba ingawa TLS ina wanachama takribani 5,000, zaidi ya nusu ni wanasheria vijana ambao wengi wao wanaelezwa kumuunga mkono Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa chama hicho.

Wanasheria hao vijana wanaelezwa kuwa na mwelekeo wa kutaka mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa taasisi hiyo na wanamwona Lissu kama mtu pekee anayewakilisha taswira hiyo ipasavyo.

Kubwa zaidi linalodaiwa kumsaidia Lissu ni hatua ya serikali kuonekana haimtaki Lissu, kiasi cha mmoja wa mawaziri wa Magufuli, Dk. Harrison Mwakyembe, kutishia kukifuta chama hicho endapo kitaendeshwa katika misingi ya kisiasa.

Dk. Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba na pia mwanasheria kitaaluma na mwanachama wa TLS alitoa tishio hilo wakati akizungumza na ujumbe wa mawakili uliomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma mapema mwezi huu.

“ Mimi nisingeweza kumchagua Lissu kuwa Rais wa TLS. Sidhani kama ni mtu sahihi kwa chama chetu. aliongea Mwakyembe. Lakini serikali ni kama imemsaidia apate nafasi hiyo na nadhani sasa atapata.

Tanganyika law society


“ Serikali imemfuatafuata sana na sasa wanasheria wanasema enough is enough. Imetosha. Mwakyembe alisema wataifungia TLS. Naona watamchagua Lissu ili waone kama ana ubavu wa kukifunga chama hicho,” alieleza mmoja wa majaji waliozungumza na muandishi wetu pasipo kutaka kutajwa majina yao.

Mmoja wa mawakili maarufu nchini, Alex Mgongolwa, aliongea na muandishi wetu juzi Jumatatu kwamba hadhani kwamba Lissu ni mgombea wa kudharauliwa katika kinyang’anyiro hicho.

“ Nadhani demography ( suala la umri) kwa sasa linampa faida mgombea anayeungwa mkono na vijana. Kwa hali ilivyo sasa, Lissu anaungwa mkono na mawakili wengi vijana ambao ndiyo wanaunda sehemu kubwa ya wapiga kura. Nadhani Lissu ana nafasi,” alisema Mgongolwa.

Kwa upande wake, wakili mwingine ambaye amewahi pia kuwa mwandishi wa habari, Aloyce Komba, alisema wapo mawakili wenye wasiwasi na Lissu lakini kuna mazingira yaliyopo sasa yanampa nafasi.

“ Siwezi kusema kwamba mimi nitampigia kura yangu Lissu lakini nasema kuna mazingira ambayo yanampa faida. Watu wanataka kuona TLS iliyo ngangari na wanadhani Lissu anaweza kuifanya hivyo.

“ Kuna suala la umri wa wapiga kura ambalo ni la muhimu. Kwenye chaguzi zote za karibuni, mgombea aliyeungwa mkono na mawakili vijana ndiye hatimaye alishinda. Kwa sasa, inaonekana upepo wa vijana uko kwa Lissu na hivyo huwezi kumdharau,” alisema wakili Komba.