Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 1:27 pm

NEWS: KENYA YATIA SAINI NA USWISI KUREJESHA FEDHA ZILIZOIBWA NA MAFISADI

NAIROBI: Kenya imetia saini mkataba na serikali ya Uswisi, ili kusaidia kuzirejesha mabilioni ya fedha za umma, zilizoibwa na kufichwa katika Benki za Uswisi na mafisadi.

Mkataba huo umetiwa saini na kushuhudiwa na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mgeni wake rais wa Uswisi Alain Berset, aliyemtembelea katika Ikulu ya Nairobi.

Rais Kenyatta amesema, anatumaini kuwa mkataba huo utasaidia kurejesha Shilingi za nchi hiyo Bilioni 72 ambazo ziliibiwa na wafanyikazi wa serikali na kufichwa nchini Uswisi, hasa baada ya kutokea kwa kashfa ya Anglo Leasing.

Aidha, ameongeza kuwa fedha hizo zikirejea zitasaidia kuendesha miradi ya serikali ikiwa ni pamoja na elimu ya bure katika shule za msingi na sekondari.

Mbali na Uswisi, fedha nyingine za wizi zinaamiwa zimefichwa katika kisiwa cha Jersey na nchini Uingereza.

Rais Kenyatta amesema, ameamua kupambana na wizi wa fedha na umma na ufisadi, kamwe hautakubaliwa katika serikali yake.

Nchini Kenya, hivi karibuni, kumeshuhudiwa viongozi mbalimbali akiwemo Gavana wa Kaunti ya Busia, akikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ufisadi, huku rais Kenyatta akisifiwa kwa kuonesha utashi wa kisiasa kupambana na ufisadi.

Makataba kama huu pia, hivi karibuni ulisainiwa nchini Nigeria na kuisaidia nchini hiyo kupata Dola Bilioni 1.2, fedha za umma zilizokuwa zimeibiwa na kufichwa nchini Uswisi.