Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 5:53 pm

News: Kamati ya Maadali yakiri Jina la Mbowe lilitajwa kimakosa na Makonda

Dar es salaam: mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu Wiliam Mwamalanga, amesema amesikitishwa na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kumtaja Freeman Mbowe kuwa miongoni mwa watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Askofu Mwamalanga alisema kamati yao ilitilia shaka Bilicanas iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya Mbowe Hotels, kwamba ni moja ya maeneo yanayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kufanya biashara zao, lakini si mwanasiasa huyo.

Alisema ukumbi huo wa starehe kuhusishwa na biashara hiyo, haikumaanisha kwamba mmiliki wake ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anahusika.

“Sisi tulisema klabu ya Bilinacas inajihusisha na uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya kwa sababu walikuwa wanaingia watu mbalimbali ambao walikuwa wakiendesha shughuli hizo, lakini hatukumtaja mmiliki wake Mbowe ndiye anayejihusisha na dawa hizo,” alisema Askofu Mwamalanga.

Alisema kamati hiyo itashirikiana na Serikali ili kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya inatokomezwa na wahusika wote wanafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Kamati hiyo pia imempongeza Rais Dk. John Magufuli kumteua Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya mwenye taaluma ya kusimamia suala hilo, jambo ambalo limesaidia kutotajwa watuhumiwa hadharani badala yake wahusika waweze kuchukuliwa hatua.