Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 3:34 pm

NEWS: IKUPA: JAMII ISIWE KIKWAZO KWA WATU WENYE ULEMAVU KUPATA HAKI YA KUOA NA KUOLEWA.

DODOMA: Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Mhe.Stella Ikupa ameiasa jamii kutokuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu kupata haki ya kuoa na kuolewa kutokana na mitazamo hasi inayowagandamiza.

Rai hiyo ameitoa wakati wa kufungua Warsha ya siku mbili Juni 28 hadi 29, 2018 iliyofanyika katika Hoteli ya Morena Jijini Dodoma.

Lengo kuu la warsha hiyo lilikuwa kujadili na kupeana mikakati ya namna bora ya ujumuishwaji, usimamizi na utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu ambapo ilihusisha Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya Watu wenye Ulemavu nchini pamoja na Waratibu wa madawati ya Watu wenye Ulemavu kutoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali.

Waziri Ikupa alieleza kuwa jamii inapaswa kubadili mitazamo hasi inayokiuka haki za watu wenye ulemavu kwani kumekuwa na mila na desturi potofu za kuwaona watu wenye ulemavu kama wasiojiweza na wasiostahiri kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu asiye na ulemavu.

“Jamii inapaswa kuwathamini na kuwapa fursa sawa watu wenye ulemavu hususan kwa kuheshimu maamuzi yao na kuwapa uhuru katika kuchagua watu sahihi wa kuishi nao pasipo vikwazo vyovyote,”alisema Ikupa

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Action on Disability and Development (ADD) Bi. Rose Tesha alifafanua umuhimu wa kuangalia makundi ya watu wenye ulemavu katika kupewa haki na usawa katika maamuzi ya kimsingi ikiwemo maamuzi ya kuchagua wenza wao katika maisha ya ndoa.

“Kimsingi ni kuangalia namna gani watu wenye ulemavu wataweza kupata fursa sawa kama aliyo mwanadamu mwingine kwa kutambua ni nini wanahitaji kufanya katika jamii yao sambamba na malengo waliyonayo, kwa kufanya hiyo itasaidia kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Tesha.

Aidha, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Jacob Mwinula aliungamkono rai iliyotolewa na Naibu Waziri kwa kuitaka jamii kubadili mitazamo inayogandamiza haki na usawa kwa wenye ulemavu ili kuwa na jamii jumuishi.

“Watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na changamoto kwenye masuala ya mahusiano ambapo jamii imekuwa kikwazo kwa kutowapa ushirikiano, hivyo jamii yetu ikiwa yenye mazingira jumuishi itasaidia kupunguza au kukomesha kabisa changamoto hizi,” Alisema Mwinula.