Home | Terms & Conditions | Help

November 30, 2024, 3:32 pm

NEWS: DALADALA DAR KUJUMUISHWA KWENYE MRADI WA UDART

Dodoma: Serekali imesema kuwa itapunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es salaam kwa kuwashirikisha na Chama cha Wamiliki wa Daladala (UWADAR) ili kuwa miongoni mwa watoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (Udart).

Akizungumza bungeni leo Mei 10, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amesema wako wawekezaji wa ndani na nje wakiwamo Uwadar wenye uwezo wa kutoa huduma muhimu na Serikali inaendelea kuondoa changamoto zilizopo sasa na kupata mwekezaji mwingine atakayeingia magari na kuufanya usafiri huo kutoa huduma kwa ufanisi.

Akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni(CCM) Maulid Mtulia, Majaliwa, amesema: “Ni kweli tuna mradi wa usafirishaji wa Udart, muungano wa Uda na Dart, Serikali inajua miundombinu yetu hasa pale makao makuu ya mabasi (Jangwani), mgogoro wa undeshaji, sehemu yoyote kunapokuwa na muungano wa taasisi mbili kunakuwa na changamoto.” Katika swali la msingi, Mtulia alitaka kujua mikakati ya Serikali kutatua mgogoro ulipo baina ya kampuni ya Udart na Maxmalipo jijini Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa jiji hilo, Majaliwa amesema wanalifanyia kazi.

“Tunaingia awamu ya pili, tunaingia na mdau mwingine ili kuwa na ushindani zaidi,” amesema Majaliwa na kusisitiza kwamba ukiwa na mwendeshaji mmoja akipata tatizo mwingine anaendelea. Waziri Mkuu amesema iwapo itabainika mwendeshaji wa sasa akawa na matatizo basi ataondolewa.