Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 2:39 pm

News: BILLICANAS ya Mbowe yaanza kubomolewa Rasmi

Dar es salaam: SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe

Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.

muakilishi media lilishuhudia ubomoaji huo ukiwa katika hatua za awali na baadhi ya vijana walionekana wakianza kuondoa vioo na vigae vilivyoezekwa katika jengo hilo wakiwa chini ya usimamizi wa walinzi.

Hata hivyo, walipoulizwa watu waliokuwa wakisimamia katika eneo hilo walidai kuwa ubomoaji huo ni wa kawaida na ulipangwa kufanyika muda mrefu na endapo waandishi watahitaji maelezo wawasiliane na uogozi wa NHC.

Akiongea na muakilishi media Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alikiri shirika hilo kuanza kubomoa jengo hilo na kusisitiza kuwa ubomoaji huo utadumu kwa muda wa siku tatu.

“Nipo likizo lakini najua kama jengo linabomolewa, ubomoaji huo umeanza leo (jana) na utamalizimika Jumapili (kesho),” alisema Mchechu.

Alipoulizwa aina ya uwekezaji uliopangwa kufanywa na NHC katika eneo hilo baada ya ubomoaji huo aliahidi kutoa maelezo hayo keshokutwa.

“Naomba tu univumilie leo (jana), jua tu tunabomoa jengo maelezo ya kinajengwa nini na kwa matumizi gani nitayatoa Jumatatu (keshokutwa), naomba tuonane siku hiyo utapata maelezo yote,” alisema Mchechu.

Mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe siku 14 kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.

Mpango huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.

Mwanasenga alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo na masuala ya siasa.