Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 5:46 pm

NEWS: BANDARI YA MTWARA YAWEKA HISTORIA KWA KUSHUSHA TANI 10,000

MTWARA: Bandari Mtwara inaingia kwenye sehemu ya historia kwa kutarajia kushusha tani 10,000 za mafuta ya petroli na dizeli ambazo ni kiwango kikubwa tangu ianzishwe. Bandari ya Mtwara ni ya tatu kushusha mafuta kwa kiwango hicho baada ya bandari za Dar es Salaam na Tanga.

Mafuta hayo yamesafirishwa kwa meli ya STI Brooklyn iliyotia nanga katika Bandari ya Dar es Salam tangu Alhamisi wiki hii ikiwa na mafuta yenye tani za ujazo 35,000, ambazo tani 10,000 zitashushwa kwenye Bandari ya Mtwara.

Bandari ya Tanga ilianza kushusha mafuta mwaka 2015, ambapo imekwisha pokea tani zaidi ya 20,000 za shehena ya mafuta ya petroli na dizeli kwa nyakati tofauti.

Miongoni mwa tani 35,000 za ujazo zilizomo kwenye meli hiyo ya STI Brooklyn, tani 28,000 ni mafuta ya petroli na tani zilizobaki 7,000 za ujazo ni mafuta ya dizeli.

Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mlali alisema ni mara ya kwanza kwa bandari yake kupokea mzigo mkubwa namna hiyo wa mafuta wa tani za ujazo 10,000 kwa mara moja. Mlali alisema bandari hiyo ilishawahi kupokea mafuta miaka minne iliyopita, lakini kwa kiwango kidogo ambacho hakikuzidi tani za ujazo 2,500.

Kwa mujibu wa Mlali, gati ya Bandari ya Mtwara ina kina cha mita 6.5 maji yanapopungua na hufikia mita 12 maji yanapojaa, hivyo isingeweza kuipokea meli hiyo ikiwa na tani zote za ujazo 35,000.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja, Erasto Simon, amesema, tani za ujazo 25,000 za petroli zitashushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia kesho na tani nyingine za ujazo 10,000 zitashushwa kwenye Bandari ya Mtwara.

Simon alisema meli hiyo inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Jumatano ijayo kwenda Bandari ya Mtwara ambako itashusha mafuta hayo siku inayofuata.

Kwa mujibu wa Simon, kati ya tani za ujazo 10,000 za mafuta zitakazoshushwa Mtwara, tani 3,000 za ujazo ni mafuta ya petroli na tani 7,000 za ujazo ni dizeli. Meli hiyo mara baada ya kutia nanga kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ililazimika kusubiri kwa kuwa kulikuwa na meli nyingine iliyokuwa ikishusha mafuta bandarini hapo.

Simon aliliambia gazeti hili kuwa kutokana na kuwepo kwa foleni ya kushusha kwenye Bandari ya Dar es Salaam, walilazimika kuwasiliana na wenzao wa Mtwara ili kujua kama Bandari ya Mtwara ina uwezo wa kuipokea meli hiyo ikiwa na mzigo wote wa tani za ujazo 35,000, ili waanze kushusha wao kwanza tani zao 10,000 na baadaye ingerudi tena Dar es Salaam kushusha tani 25,000 za ujazo.

Alisema kwa kuwa alihakikishiwa na wenzao wa Mtwara kuwa gati yao haina uwezo wa kupokea mzigo wote huo kwa mara moja, ndipo meli hiyo imelazimika kuendelea kusubiri zamu yake ya kushusha kwenye Bandari ya Dar es Salaam kabla ya kuondoka kwenda Mtwara Jumatano.

“Meli hii ni ya kawaida, siyo kubwa sana, na kutokana na foleni, tuliongea na wenzetu wa Mtwara tuone kama bandari yao ina uweza kuipokea meli hii ikiwa na tani zote 35,000 za ujazo ili wao wangeanza kushusha kwanza hizo tani 10,000 na baadaye ingerudi hapa Dar es Salaam, nasi tushushe tani zetu 25,000, lakini waliniambia gati yao haina uwezo huo,” alisema Simon.



chanzo habari leo