Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 5:38 pm

MLIPUKO ETHIOPIA: MAAFISA 9 WA POLISI WAKAMATWA AKIWEMO MKUU WA POLISI

Addis ababa: Mamlaka ya serekali nchini Ethiopia zinasema kuwa maafisa tisa wa polisi, ikiwa ni pamoja na naibu mkuu wa polisi mjini Addis Ababa, wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Shirika la habari la BBC, liliripoti kwamba maafisa hao wa polisi wanafanyiwa uchunguzi "kwa kukosa kudhibiti eneo hilo la mkutano ambapo mlipuko huo ulitokea."

Waziri mkuu Abiy Ahmed ambaye kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters - ameleta mabadiliko makubwa ya kiutawala, alikuwa tu amemaliza kutoa hotuba yake wakati guruneti hiyo ilipolipuka.

Maafisa wa wizara ya Afya nchini Ethiopia walisema Jana Jumapili kuwa mtu wa pili alikufa kufuatia mlipuko uliotokea hapo Jumamosi wakati wa mkutano uliohutubiwa na waziri mkuu huyo, kwenye mji mkuu, Addis Ababa.

Maafisa wa serikali walisema watu 150 walijeruhiwa na mlipuko huo.

Abiy alisema shambulizi hilo lilikuwa limepangwa na kwamba polisi wanachunguza ni nani aliyehusika.

Katika mahojiano ya televisheni Jumamosi, Abiy alisema upendo utashinda na kwamba kujaribu kuwaua watu si kuonyesha ushupavu.

"Wale waliojaribu kuwagawanya Waethiopia hawakufaulu," aliongeza.

Abiy alichukua usukani mwezi Aprili na amefanya mabadiliko mengi, ikiwa ni pamoja na kuwaachilia wafungwa wa kisiasa na waandishi wa habari.

Kadhalika ameanzisha mikakati ya uimarishaji wa uchumi huru na kuahidi kutafuta mwafaka wa amani kati ya Ethiopia na hasimu wake, Eritrea.