- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
MAKALA: MPENDE AU MCHUKIE ZITTO KABWE ANAENDELEA KUWA MWANASIASA ADIMU
Inaandikwa na Evarest Chahali
Mpende au mchukie, Zitto Kabwe anaendelea kuwa mmoja wa wanasiasa adimu kabisa katika siasa za Tanzania yetu. Na kila mwenye uchungu wa dhati kwa Tanzania yetu anapaswa kumuunga mkono.
Ni rahisi kumchukia kuliko kumpenda. Kwa sababu ni rahisi kutokuwa na sababu za kutompenda mtu. Na ni rahisi zaidi kumchukia mtu “aliyekamilika takriban kila idara.”
Lakini hata kama ni rahisi “kumchukia bila sababu” au kwa vile tu “yupo vizuri” (watu wazuri ni serial victims wa wenye chuki) ni ngumu mno kuhalalisha chuki dhidi yake. Ni vigumu kumchukia mtu aliyejitolea sehemu kubwa ya maisha yake sio tu kuwa msemaji wako bali pia mpiganaji mahiri dhidi ya wanaopora/wanaokandamiza haki zako.
Mie namfahamu Zitto kitambo. Tangu akiwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nnachoweza kusema “bila kuvunja miiko ya siri” ni kwamba “alitusumbua sana” (enzi hizo za utumishi wangu serikalini).
Sio kwamba “alitusumbua” kwa sababu alikuwa mhalifu, au alikuwa akivunja sheria za nchi. Hapana. Zitto alikuwa mwanaharakati “mwiba kwa serikali.” Na kama ujuavyo kuhusu serikali nyingi za Kiafrika, mtu anayejitolea kupigania haki za wengine huonekana kama “adui wa taifa.”
Na kwa kiasi kikubwa, Zitto amebaki kuwa mtu yuleyule, japo sasa ni mwanasiasa kamili tofauti na enzi hizo alipokuwa mwanaharakati kamili. Na yayumkinika kusema kuwa Zitto anachanganya siasa na uanaharakati katika namna ambayo yeye tu anaweza, na kwa ufanisi usio na mfano.
Sie Waswahili ni wagumu sana kusifia japo wepesi sana “kuponda.” Tathmini ya haraka haraka tu inaweza kumfahamisha Mtanzania yeyote yule kuwa mchango wa Zitto katika mustakabali wa taifa letu ni mkubwa mno.
Na kwa miaka kadhaa sasa, amejipa jukumu la kutufanyia uchambuzi wa ripoti za CAG. Na sio uchambuzi wa juujuu bali wa kina mno. Unajua mara nyingi hizo ripoti huandikwa kama machapisho ya kitaaluma, na kwa wananchi wengi wa kawaida ni ngumu kuelewa kilichomo.
Majuzi amefanya tena kazi kubwa kutufahamisha kuhusu shilingi trilioni moja unusu ambazo CAG anatanabaisha kuwa “hazijulikani zilipo.” Sasa huhitaji kuwa mjuzi sana kubaini kwamba kiasi kikubwa cha pesa kama hicho hakiwezi “kutojulikana kilipo” hivihivi tu.
Na kwa vile Rais John Magufuli amejitambulisha kama mpambanaji dhidi ya ufisadi basi tulitarajia yeye na serikali yake na chama chake waunge mkono jitihada za Zitto kuhusu “kupotea” kwa fedha hizo.
Badala yake, Zitto amekuwa akiandamwa kana kwamba yeye ndo aliyechaoisha ripoti ya CAG inayoeleza bayana kuwa haieleweki trilioni moja unusu hizo “zimejificha” wapi.
Tukiweka kando kuandamwa na Magufuli na serikali yake na chama chake, kwa kiasi kikubwa Watanzania nao tumemwangusha. Tumemwangusha kwa sababu uchambuzi wa kina alioufanya kuhusu ripoti ya CAG ulipaswa kutuamsha na kutambua kuwa “Magufuli na walewale” na serikali yake ni ya “CCM ileile.”
Kwamba hizo filimbi za kupambana dhidi ya ufisadi zinaweza kuwa njia ya kuficha ufisadi mkubwa zaidi ya tuliowahi kushuhudia huko nyuma.
Halafu hata kama Zitto asingetufumbua macho, busara kidogo tu zilipaswa kutuamshia maswali kuhusu maeneo yenye utata kama “ujenzi wa uwanja wa ndege ya kimataifa huko Chato” (kioja cha karne) na ununuzi wa (+kukomboa) bombadia.
Wakati huu ninapoandika makala hii, mjadala kuhusu hatma ya Shilingi trilioni moja unusu “zisizojulikana zilipo” ni kama umefungwa. Sio na serikali, sio na CCM, wala sio na Magufuli, bali sie tuliopaswa kuenzi jitihada binafsi za Zitto na Chama chake, sambamba na kazi nzuri ya CAG na “kulishikia bango” suala hilo.
Kuna watakaokurupuka na kudai “hizo ni chuki dhidi ya Magufuli.” Hapana. Hizo ni chuki dhidi ya ufisadi. Na hata kama Magufuli anatamani kuwa kiongozi wa malaika huko mbeleni, haimaanishi tumwache tu atumie pesa za walipakodi kadri atakavyo, na apuuze taratibu za kibajeti zinazolazimisha kuidhinishwa kwa matumizi mbalimbali.
Wengine waliotuangusha ni nchi/mashirika wahisani. Angalau naweza kuelewa kwanini Uingereza imekuwa “ikimwonea aibu Magufuli.” Taarifa nilizonazo ni kwamba Uingereza inaiona Tanzania kama fursa nzuri kwake baada ya kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit), na kumekuwa na jitihada kubwa za kufumbia macho “madhambi ya Magufuli” hususan ukandamizaji wa demokrasia na udikteta wa waziwazi.
Hata pale yule “msemaji asiye rasmi wa Serikali” Musiba alipodai kuwa Uingereza ni miongoni mwa nchi zinazowafadhili “watu hatari” nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa wafadhili wakuu wa Tanzania haikutoa tamko lolote.
Hali ni hivyo hivyo kwa Canada, Ujerumani, Marekani na Denmark ambazo pia zilitajwa kutufadhili tunaoitwa “watu hatari.”
Bila kuvunjwa moyo na tulivyomwangusha katika suala la shilingi trilioni moja unusu zilizotanabaishwa katika ripoti ya CAG, Zitto amejitoa mhanga kwa mara nyingine na kutufahamisha kuhusu mamia ya watu “waliopotea” huko Mkiru.
Sie Watanzania ni watu wa ajabu sana. Hivi inawezekanaje mamia ya wenzetu “wapotee” pasipo kutuhangaisha sie tunaojinadi kuwa “Kisiwa cha amani na utulivu”?
Wakati flani, IGP Sirro (hivi yu wapi huyu bwana?) alitamka kuwa kuna watoto 1300 hawajulikani walipo huko MKIRU. Lakini kama kawaida yetu, tukapuuza. Sie ni wazuri mno kwa kupuuza vitu vya muhimu. No wonder, empty brain Daudi Albert Bashite bado anakalia kiti cha enzi, de-facto President, na mtu mwenye nguvu kubwa kuliko wote Tanzania, except babake. Tumefikaje hapa kama taifa?
Turejee kwenye suala la MKIRU. Licha ya jitihada za Zitto kuweka hadharani takwimu zilizopo kuhusu idadi ya watu “waliopotea” 380 hadi sasa, hakuna hasira yoyote miongoni mwa wananchi kuhusu suala hili.
Ofkoz, kama Kamanda Sirro aliposema kuna watoto 1300 hawajulikani waliko na hakuna aliyejali, sembuse hao 380!?
Inaudhi. Inakera. Inachukiza. Inavunja moyo. Inasikitisha.
Na kwenye vyama vya upinzani, kwa upande wa Chadema ni kama Magufuli amefanikiwa kutimizs azma yake ya kuuwa upinzani, maana sio tu inashangaza kuona chama hicho kikuu cha upinzani kikiwa kimya kuhusu shilingi trilioni moja unusu “zisizojulikana zilipo” lakini pia wamekalia kimya suala la MKIRU.
Na ukisikiliza kauli za baadhi ya wabunge wa chama hicho — Peter Msigwa, Peter Lijuakali, Susan Kiwanga na Profesa Jay - walipokutana na Magufuli kwenye ziara zake, ni wazi kwamba Chadema si wa kuaminika katika mapambano dhidi ya udikteta wa Magufuli.
Kama kuna mwanasiasa mmoja wa Chadema ambaye bado anapigana kufa na kupona ni John Heche ambaye majuzi tu amempoteza mdogo wake aliyeuawa na polisi kwa kisu.
Akina Msigwa na wenzake wamesahau kabisa kwamba muda huu ninapoandika makala hii, kuna mbunge mwenzao amatumikia kifungo kwa sababu tu ya chuki za kisiasa za Magufuli. Licha ya Mbunge huyo, Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu, kuna lundo la makada wa chama hicho waliopo jela huku lundo jingine likikabiliwa na kesi mbalimbali.
Ukimweka kando Heche, Chadema imeshindwa kabisa kuziba pengo la wanasiasa kama Dokta Slaa na Zitto waliojiondoa katkka chama hicho huko nyuma, na pia wameonyesha bayana kuwa ni “wepesi” bila Tundu Lissu anayepata matibabu nchini Ubelgiji baada ya kunusurika kuuawa.
Na tukimtaja Lissu unaweza kupatwa na hasira kwa jinsi Chadema walivyoamua kupuuzia jaribio hilo la mauaji dhidi ya mbunge wake hiyo aliyekitumikia chama hicho kwa nguvu kubwa.
Ila Chadema wakae wakielewa kuwa kama ilitokea kwa Kamanda Mashaka, ikatokea kwa Diwani Luwena na ikatokea kwa yule kada wao wa Hananasifu jijini Dar, ambao wote waliuawa kinyama, na kama imetokea kwa “kupotea” kwa Ben Saanane sambamba na jaribio la kumuuwa Lissu mchana kweupe, hakuna aliye salama katika chama hicho. Labda usalama wao pekee ni hii hali waliyoamua kujiweka sasa, kutia pamba masikioni na kujifanya kama hawana habari kuhusu trilioni moja unusu au MKIRU.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu umuhimu wa kuyapa kipaumbele masuala muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Japo sitarajii kuona mtu kama Zitto akiamua kukata tamaa au kuachana na utetezi wake kwa Watanzania wasiojali yanayowasibu, lakini kama mwanadamu mwingine anaweza kuvunjika moyo na pengine kuelekeza nguvu kwenye kujenga chama chake cha ACT Wazalendo ambacho kina potential kubwa tu ya kuwa mbadala wa Chadema kama chama kikuu cha upinzani.
Nihitimishe makala hii kwa kumpongeza sana Zitto kwa kujitolea kuwa msemaji na mtetezi wetu, huku wakati mwingine akihatarisha maisha yake. Tupo tunaothamini mno jitihada zako na tuna imani zitazaa matunda. Katika hili la MKIRU, naahidi kukuunga mkono kwa nguvu zangu zote kwa sababu “huyo aliyekwishakunywa damu za watu hao 380 ataendelea kunywa damu nyingi zaidi pindi asipodhibitiwa.” Kasumba ya Watanzania kupuuzia masuala ya msingi huwafanya watawala dhalimu kujiona kama wamepewa ridhaa na wanaowaongoza, maana hakuna hasira wala hatua dhidi ya udhalimu wao