Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 2:20 am

KAMANDA MAMBOSASA: HAKUNA MBUNGE HATA MMOJA ALIYERIPOTI OFISI YA UPELELEZI DAR

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema kwamba mpaka sasa hakuna Mbunge yeyote aliyopo Dar es salaam aliyeripoti kwenye ofisi ya Mpelelezi wa kanda hiyo, kutokana na kukiuka kwa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda, aliyewapa masaa 24 kurudi Bungeni kuendelea na Majukumu yao.

Kauli hiyo Kamanda Mambosasa ameitoa leo Mei 9, 2020, wakati akizungumza na kituo cha runinga cha EATV.

Kituo hicho kilitaka kufahamu kama kuna Mbunge yeyote aliyeripoti kwa hiyari yake kama ambavyo Jeshi la Polisi lilivyoagiza siku ya Mei 7 baada ya agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda.

"Hakuna hata mmoja aliyeripoti, inawezekana hawapo Dar es Salaam na ndiyo maana nilisema kama kuna yeyote bado yupo, na hakuna aliyepatikana pia, hatujawasaka lakini ule ulikuwa ni wito" amesema Kamanda Mambosasa.

Siku ya Mei 6, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitoa muda wa saa 24 kwa Wabunge ambao wako Jijini humo, waondoke na kurejea Dodoma kuendelea na shughuli zao za Bunge na atakayekaidi kufanya hivyo basi atakamatwa kwa kosa la uzururaji kama wanavyokamatwa machangudoa nyakati za usiku.

Lakini baada ya Kipindi hicho kupita Jeshi la Polisi Kanda maalum Dar es salaam lilitoa wito kwa wabunge wote walioko Dar es salaam kuripoti katika ofisi ya mpelelezi kanda maalumu ya Dar es salaam.