Home | Terms & Conditions | Help

April 1, 2025, 1:16 pm

NEWS: SERIKALI YASHAURIWA KUACHA UTEGEMEZI DAWA ZA UKIMWI

DODOMA: WAJUMBE wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI wameiomba Serikali kuondokana na utegemezi wa fedha za wafadhili kwenye Mfuko wa Ukimwi kwa kuweka tozo maalum ya Shilingi 10 ili kufikia malengo ya kupambana na ugonjwa huo.

Wakichangia mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo Mbunge wa Bahi Omary Badwel,wabunge wa viti maalum Martha Mlata na Zaynabu Vulu wamesema ni muhimu kwa Serikali kuwajibika kikamilifu katika mapambano ya ugonjwa huo.

Akijibu hoja zilizotolewa na wabunge katika kikao hicho Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na Watu wenye ulemavu Jenista Mhagama amesema mfuko huo ni muhimu katika mapambano ya UKIMWI nchini na Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha kunakuwepo na vyanzo vya kutosha kwenye mfuko huo ili uweze kujiaendesha.

Awali, Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dokta Leonard Maboko akiwasilisha taarifa ya mfuko huo ameiomba Serikali kuweka mikakati madhubuti ili mfuko huo uweze kujitegemea.

Mfuko huo ulizinduliwa Mwezi Desemba 2016 lengo likiwa ni kusaidia jitihada za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI nchini.